Breaking

Friday, 3 June 2022

WABUNIFU UDSM WANAVYOTUMIA BIOTEKNOLOJIA KUMKOMBOA MTANZANIA




Na Mwandishi Wetu


WANAFUNZI wabunifu za bioteknolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Ndaki ya Sayansi ya Asili na Sayansi Tumizi wameomba Serikali kuwawezesha ili waweze kuendeleza bunifu zao.

Ombi hilo wamelitoa jana wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hii alipowatembelea chuoni hapo na kuona ubunifu waliofanya kwa njia ya bioteknolojia.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu Danford Danford anayesoma Shahada ya Molekuli ya Biolojia na Bayoteknolojia alisema wanafunzi wamekuwa wakibuni bunifu nyingi ila wamekuwa wakikwama kuziendeleza.

Danford alisema yeye amebuni utengenezaji wa Karagenan (Carrageenan) kwenye zao la mwani kwa njia ya bioteknolojia hali ambayo itawezesha kuongeza thamani ya bidhaa hiyo ambayo ni muhimu kwa wenye viwanda na wafanyabiashara kwa ujumla.

“Mimi nimetumia bakteria ambao wapo kwenye zao la Mwani na kutengeneza Karagenan hapa hapa nchini, hivyo iwapo ubunifu wangu huu utapewa kipaumbele utaweza kumkomboa mkulima ambaye anauza Mwani kwa bei ndogo,” alisema.

Mbunifu huyo wa kutengeneza Karagenan kwa njia ya bioteknolojia alisema kwa sasa kilo moja ya mwani inauzwa Sh.800 ambapo inapelekwa nje na kurejeshwa kama Karagenan.



Alisema bidhaa hiyo ya Karagenan inatumiwa kwenye kutengeneza vipodozi, sosoji, barafu na bidhaa nyingine, hivyo anaomba Serikali na taasisi nyingine kuwawezesha ili kuongeza thamani ya mwani hapahapa nchini.

“Ubunifu wetu huu unaenda kuongeza mnyororo wa thamani wa mwani ambapo Tanzania inavuna zaidi za tani laki moja kwa mwaka, ila wote unauzwa nje ya nchi,” alisema.

Kwa upande wake David Kazuguri mbunifu wa mbolea halisi ya mazao kwa njia ya bioteklojia alisema iwapo watapewa sapoti na Serikali wataweza kukomboa mkulima ambaye amekuwa akiteseka kwa bei kubwa ya bidhaa hiyo.

Kazuguri alisema mbolea hiyo ambayo wameitengeza kwa njia ya bioteknolojia inatokana na takataka za aina mbalimbali kama maganda ya viazi, ndizi, mchicha na mazao mengine yanayopatikana sokoni.



“Changamoto ya mbolea nchini imesababisha sisi kuja na ubunifu huu, tumetumia bakteria, fangasi na vidudu nukta vingine ambavyo vinatumika kuchakata mchakato wa mbolea hii kupatikana,” alisema.




Alisema iwapo watafanikiwa kupata mtaji wa kuanzisha kiwanda watawezesha kuajiri vijana wengi wa Waranzania, hivyo wanaomba Serikali kuwawezesha.

Naye Mbunifu Daud Nzunda alisema wao wamebuni jiko ambalo linatumia mabaki ya mimea na wanyama, hali ambayo itapunguza uzalishaji hewa ukaa.

Mwanafunzi huyo wa Shahada ya Molekuli ya Biolojia na Bayoteknolojia alisema jiko hilo litawezesha wananchi wa vijijini kupata nishati ya umeme wa uhakika kutokana na vyanzo kutoka kwenye maeneo yao.

“Wakulima wanalima wanavuna mahindi, maharage na mazao mengine tumeona tutumie bioteknolojia kuwasaidia wananchi hasa wa vijiji kupata nishati safi na salama na kwa gharama nafuu kupitia mabaki ya mzao hayo,” alisema.

Akizungumzia ubunifu hizo za wanafunzi Mratibu wa Huduma ya Jamii na Maarifa wa Ndaki ya Sayansi ya Asili na Sayansi Tumizi, Dk. Ally Mahadhy alisema wanachofanya wanafunzi hao ndio lengo la UDSM kuibua vipaji ili kusaidia jamii.

“Bunifu hizi zinaonesha ushahidi tosha kuwa Ndaki yetu na UDSM kwa ujumla tunapika vijana ambao wakitumika vizuri wanaweza kukomboa jamii ya Kitanzania,” alisema.

Dk. Mahadhy alisema chuo kitaendelea kuwasaidia maarifa wanafunzi wote ambao watakuja na ubunifu mpya ukiwemo wa kutumia bioteknolojia ambayo ndio inashika nafasi katika dunia kwa sasa.

Mwisho

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages