Breaking

Tuesday, 28 June 2022

ULINZI WA PAKA DHAHABU KUONGEZWA ILI KUTHIBITI KUTOWEKA KWAKE



Na Lydia Lugakila, Lango la habari


Mhifadhi wa misitu shamba la miti Rubare  mkoani Kagera Hamidu Miraji Shaluwa amesema ulinzi wa paka wa dhahabu utaimarishwa ili kudhibiti kutoweka kwake.


Shaluwa  amesema kuwa paka dhahabu ni mnyama anapatikana msitu wa hifadhi wa minziro wilayani Misenyi mwenye uwezo wa kuishi kati ya miaka 15 anakuwa na uzito wa kg 5.5 - 16 akiwa mdogo na urefu wake kwenda juu ni cm 38-55.


Amesema kuwa tayari wameongeza ulinzi kwa watu wasiopenda kufuata sheria,na kuwa paka huyo yupo  hatarini  kutoweka iwapo shughuli za kibinadamu hazitasitishwa ikiwemo uwindaji haramu wa wanyamapori, uchomaji moto wa misitu, kulisha mifugo ndani ya hifadhi, kukata kuni au magogo ndani ya hifadhi.


" Paka dhahabu aligunduliwa na jopo la wanasayansi wa kitanzania na wa nchi ya Italia kuwepo kwenye ardhi ya Tanzania tangu mwaka 2018 kabla ya hapo hapakuwahi kuwepo kwa taarifa yoyote ya uwepo wake" alisema Shaluwa.

Akimwelezea paka huyo amesema ni mwenye asili ya chui wadogo wadogo mwenye madoa hapendi kuchangamana,  chakula chake ni wanyama wadogo wadogo, Samaki,Pimbi, digidigi na ndege huku jina lake la PAKA DHAHABU likitokana na rangi yake na manyoya yanayofanana na rangi ya dhahabu asili ya chui .


Kupitia maonyesho hayo ya kibiashara yanayoendelea Mkoani Kagera mhifadhi huyo amewahimiza wananchi Mkoa humo na  watanzania kwa ujumla kutembelea banda la wizara ya maliasili na utalii pamoja na idara nyingine  kuendelea kujifunza utunzaji wa maliasili,  misitu,  wanyamapori kwa ajili ya kupata mazao ya misitu, chakula na kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Aidha ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na biashara yoyote ya ujangili inayoweza kusababisha kutoweka kwa vivutio hivyo.


Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwahimiza watanzania na wananchi Mkoani Kagera kutumia muda wao mwingi kutembelea vivutio vilivyopo katika maeneo yao.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages