Breaking

Monday, 27 June 2022

UHAMIAJI, TRA WATAKIWA KUTOA ELIMU KWA WAFANYABIASHARA KUONDOA VIKWAZO MIPAKANI

Na Lydia Lugakila, Lango la habari


Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania zimetakiwa kuanza utaratibu wa kutoa elimu kwa wafanyiashara walioko mipakani ili kuondoa changamoto wanazokumbana nazo. 


Maelekezo hayo yametolewa na mkuu wa wilaya ya Muleba Mkoani Kagera Toba Nguvila kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Kagera katika ufunguzi wa maonyesho ya kwanza ya kibiashara ya jumuiya ya Afrika mashariki yanayoendelea katika viwanja va CCM Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.


Kauli hiyo  imekuja kufuatia maelezo ya  mratibu wa maonyesho ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya utalii Bwn William Rutta katika taarifa iliyobainisha kuwepo kwa vikwazo ikiwemo vizuizi mipakani kwa wafanya biashara.


Dc Nguvila amemuelekeza Meneja mamlaka ya mapato Tanzania na idara ya uhamiaji Mkoa wa Kagera kuanza mara moja utaratibu wa kuelimisha wafanya biashara ili kuwapunguzia vikwazo na changamoto wanazopata kutokana na kutokuwa na elimu ya kibiashara.


" naelekeza idara hizo toeni elimu na kupokea changamoto ili kupunguza vikwazo, kuanzia sasa wekeni banda katika maonyesho haya  najua Kuna changamoto ambazo wafanya biashara wa nje wamezipata wakati wakija Mkoani hapa ikiwemo vizuizi na ambazo wafanya biashara wa ndani wanaweza kukumbana nazo wakiwa wanaenda nje"alisema mkuu huyo wa wilaya.


Ameongeza kuwa si vyema viongozi kuwa vikwazo bali wawe fursa ya kuwawezesha wafanya biashara kufanikiwa zaidi.


Aidha amepiga marufuku vitendo vya Rushwa mipakani , tozo zisizo na maana, badala yake vitumike vibali vya kisheria ambavyo haviwaletei madhara wala kuwaumiza wafanya biashara.


Ametumia fursa hiyo kuwahimiza wana Kagera na watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa za kibiashara na kukuza uchumi huku akiwasihi waandaaji wa maonyesho hayo kuwa na maono mapana ya kutoa elimu ya kibiashara kwa wajasiliamari ili kuongeza uelewa kati yao na mataifa mengine, kuandaa makongamano na wenye mitaji mikubwa kuwekeza zaidi katika kusimika viwanda.


Kwa upande wake mratibu wa maonyesho hayo William Rutta amesema vikwazo mbali mbali vikiondolewa wafanya biashara watafanya biashara zao kuwa uhuru zaidi.


Amesema kuwa lengo la maonyesho hayo ni kumuunga mkono Rais Samia ambaye amefungua milango ya nchi kwa kuleta wageni  tofauti tofauti wenye kutalii na kufanya biashara ikiwa ni pamoja na kuwezesha Mkoa huo kujinasua katika nafasi mbaya kiuchumi.


Hata hivyo mratibu huyo amesema kuwa hadi Sasa tayari wafanya biashara kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Burundi, DRC Congo, Kenya, Uganda, Rwanda tayari wako Mkoa humo kwa ajili ya maonyesho hayo.


Maonyesho hayo yameanza juni 15 na kufunguliwa rasmi juni 25, na yatafungwa julai 10, 2022 yakiwa yamebeba kauli mbiu isemayo "VIWANDA BIASHARA NA UTALII NI NGUVU KUBWA YA UCHUMI KWENYE SOKO LA AFRIKA YA MASHARIKI TUICHANGAMKIE"

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages