Na Said Muhibu, Lango La Habari
Timu ya Taifa ya Uganda Crested Cranes imetwaa ubingwa katika fainali ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Senior Challenge ya wanawake baada ya kuifunga timu ya Taifa ya Burundi kwenye mchezo uliochezwa leo June 11, 2022 nchini Uganda.
Mchezo ulianza kwa kasi sana huku mashambulizi yakipelekwa zaidi upande wa timu ya Taifa ya Burundi na ilipofika dakika ya 2' mchezaji wa Crested Cranes Sandra Nabweteme alitikisa nyavu za lango la timu ya Taifa ya Burundi, kabla ya kutamatika kwa kipindi cha kwanza Fazila Ikwaput alifunga bao la pili na kutamitisha kipindi cha kwanza Uganda ikiwa kifua mbele kwa 2-0.
Kipindi cha pili kilionesha kiu ya Burundi katika kubeba kombe huku mchezaji wao Joelle Bukuru akiwapatia goli la kwanza la mapema, ijapokuwa Uganda ikawavunja moyo dakika za mwisho kwa mfungaji wa bao la kwanza Sandra Nabweteme kutikisa nyavu za lango la Burundi kwa mara ya pili na mpira kutamatika kwa Uganda kushinda 3-1.
Aidha, kwa upande wa timu ya Taifa ya Tanzania Twiga stars imefungwa 2-1 dhidi ya timu ya Taifa ya Ethiopia katika mchezo wake wa kuwania nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo.
Magoli ya timu ya Taifa ya Ethiopia yamefungwa na Turist Lema na Tadesse Bizuayehu huku goli la kufutia machozi kwa Twiga stars likifungwa na Oppa Clement.