Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameipongeza timu ya Yanga kwa kutwaa kombe la katika ligi Kuu ya NBC katika msimu huu.
Mhe. Mchengerwa ameipongeza Klabu ya Yanga kwa kuchukua Ubingwa huo huku akipongeza mshikamano na furaha za mashabiki, ambazo wamezionyesha wakati wa kukabidhiwa kombe hilo na mapokezi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
" Kwa aina ya shangwe za ubingwa zilizofanyika jana na leo ni sawa na zile za mataifa yaliyoendelea ya Ulaya. Hakika mpira wa miguu ni mchezo mkubwa na pendwa duniani ambao huwaunganisha watu pamoja na kuleta amani, mshikamano, furaha na umoja baina ya wananchi"
Ameongeza kuwa watanzania zaidi ya 90% ni wapenzi wa mchezo wa soka na amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha inaboresha miundombinu ya michezo na kuleta usawa katika michezo hasa mpira wa miguu ili kila mtanzania aweze kupata furaha.
"Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa watanzania wanaendelea kupata furaha na faraja katika michezo" amesisitiza Mhe . Mchengerwa