Na John Mapepele, Dar es Salaam
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na michezo.Mhe, Mohamed Mchengerwa ameitaka Timu ya soka ya walemavu ya (Tembo Warriors) kutumia mechi za maandalizi na nchi mbalimbali za Ulaya kujinoa ili kushinda kombe hilo na kulirejesha nchini.
Mhe Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Juni 8, 2022 uwanja wa Benjamini Mkapa wakati akiikabidhi bendera ya Taifa timu hiyo akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi inayokwenda kuanza kucheza mashindano kwenye maandalizi na timu mbalimbali za Ulaya kwa kuanzia na timu ya Poland ili kuweza kupata uzoefu wa kucheza na nchi za mabara mbalimbali kabla ya kuanza mashindano haya.
“Tumeamua kama Serikali kuendelea kuhaakikisha kuwa tunazisaidia timu zinazofanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ili kuwasaidia kukuza ajira na kuwafanya waajiriwe kwenye vilabu vikubwa duniani” amefafanua Mhe. Mchengerwa
Amesema watanzania wamechoka kuona kuwa nchi inasuasua kwenye michezo na amesisitiza kuwa wakati huu watanzania wanataka kombe la dunia kuja Tanzania ambapo amesema hilo litafanikiwa kwa kuweka mbele utaifa na uzalendo wanapokuwa kwenye mashindano haya.
Ameongeza kuwa jambo kubwa kwa sasa ni kuwa na nidhamu na kuzingatia misingi ambayo wanapewa na makocha wa timu zao ili waweze kufika mbali na kuboresha maisha yao na uchumi wan chi yetu kwa ujumla.
“Naomba kuwaambia mkifanya vizuri katika mashindano haya ya maandalizi tu nina uhakika mtanunuliwa na timu kubwa na mtabaki ulaya, mtabadilisha maisha ya familia zenu na watanzania kwa ujumla” ameongeza Mhe. Mchengerwa
Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa timu hiyo wamemwahidi Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuwa wanakwenda kuanza kutema cheche katika maandalizi ya timu hizo za awali ili kujihakikishia kutwa kombe hilo.
Katibu Mkuu. Dkt, Abbasi amesema Tembo Warriors ndiyo timu ya kwanza nchini kufuzu kuingia kwenye mashindano hayo na kuitaka kuendelea kushikilia heshima hiyo kwa kuwa timu ya kwanza kurejesha kombe nyumbani.