Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo imeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan la kufanya Tamasha kubwa la kitaifa la Utamaduni ambalo linakwenda kushirikisha zaidi ya wadau elfu ishirini.
Akizungumza kwenye kikao cha maandalizi cha pamoja baina ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema tamasha hilo la kihistoria linajumuisha mikoa yote ya Tanzania linatarajia kuanza Julai Mosi mwaka huu katika uwanja wa Uhuru ambapo maonesho mbalimbali ya vyakula na ngoma za asili.
Amefafanua kwamba Julai, 2, 2022 kutakuwa na matembezi maalum ya kuzunguka jiji la Dar es Salaam kwenye madaraja yote ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Kasssim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kwa upande mwingine, Yakubu amesema siku ya Julai 3, 2022 itakuwa siku maalum ya miondoko ya taarabu utakaofanyika eneo la ufukwe wa Coco pembezoni mwa Bahari ya Hindi ambapo Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Tulia Ackson anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Amesema tamasha hilo pia litapambwa na vikundi mbalimbali maarufu vya taarabu kutoka ndani na nje ya nchi ambapo amesema vikundi vitano vinatoka Zanzibar, vikundi vingine vitano kutoka Tanzania bara huku vikundi vingine vikitokea Comoro, Burundi na Mombasa nchini Kenya.
Amevitaja vikundi kutoka Zanzibar kuwa ni pamoja na zahati zamani, Nadikhwan safaa, wapendanao modern culture, kikundi cha culture, chama cha wasanii wa muziki Zanzibar.
Kwa upande wa Tanzania bara ni pamoja na Jahazi modern taarab, First Class, Wana nakshinakshi, Bablom na East Africa Melody na wasanii binafsi maarufu pia wamealikwa.