Breaking

Thursday, 30 June 2022

TAKWIMU SAHIHI ZA WATU WENYE ULEMAVU KUSAIDIA UTUNGWAJI WA SERA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene akizungumza katika Kongamano la Kuwajengea Uelewa Watu Wenye Ulemavu kuhusu Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Ukumbi wa Jakaya Convention Centre Jijini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Ummy Nderianaga akifafanua jambo katika Kongamano hilo.
Baadhi ya Washiriki wakifuatilia Kongamano la Kuwajengea Uelewa Watu Wenye Ulemavu kuhusu Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Ukumbi wa Jakaya Convention Centre Jijini Dodoma.

############################# 


Na Mwandishi wetu- Dodoma


Serikali imesema upatikanaji wa takwimu sahihi za msingi za Watu Wenye Ulemavu zitawezesha kutungwa  kwa sera wakilishi na kusaidia kupima utekelezaji wa malengo mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa.


Hayo yamesemwa  Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazri Mku Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene  kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa katika  Kongamano la Kuwajengea Uelewa Watu Wenye Ulemavu kuhusu Sensa ya Watu na Makazi  ya mwaka 2022.


Mhe. Simbachawene alisema  kwa mujibu wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG)  yote imeweka mkazo katika kuhakikisha Watu Wenye Ulemavu sio tu wanakuwa sehemu ya mipango ya maendeleo ya nchi bali  wanapewa kila fursa za kujiendeleza katika nyanja zote za maendeleo kama wananchi wengine.


“Katika kuhakikisha kuwa jamii ya Watu Wenye Ulemavu wanakuwa sehemu ya mchakato mzima wa Sensa ya Watu na Makazi, Serikali imezingatia ushiriki wao katika hatua zote za utekelezaji wa zoezi hili la kitaifa. Ushiriki wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) ni ishara ya ujumuishaji huo,” alisema Mhe. Simbachawene.


Pia aliitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania Bara, na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Tanzania Zanzibar kuendelea kuboresha mbinu za ukusanyaji wa taarifa za hali ya ulemavu nchini, kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na Watu Wenye Ulemavu kwa lengo la kuwatambua na kuwahudumia.


“Ofisi za takwimu ziendelee kujumuisha maswali yanayolenga kupata taarifa za hali ya ulemavu nchini kwenye tafiti mbalimbali zinazofanywa na Ofisi hizo na Ofisi ya Waziri Mkuu ione  uwezekano wa kuanzisha mfumo wa Kiutawala wa Kukusanya Taarifa za Hali ya Ulemavu Nchini,” alieleza


Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga aliishukuru Seraikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali watu wenye ulemavu akisema kuwa wako tayari kufanya kazi kuhakikisha Taifa linakuwa na maendeleo yenye mchango wa makundi yote.


Aidha  Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa ,alibainisha kwamba Ofisi ya Taifa ya Takwimu imejipanga kuhakikisha wanachukua taarifa sahihi kwa watu wenye ulemavu itakayosaidia serikali kutambua idadi na mahitaji yao


“Tumeweka maswali ya kutosha zaidi ya maswali kumi ambayo yatatusaidia kujua kwamba nani mlemavu wa aina gani,yuko wapi ,elimu yake,mahali anapoishi, ana rasirimali kiasi gani yote”alisema


Mwenyekiti shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Bwa. Ernest Kimaya amesema lengo la kongamano hilo ni kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ili kuwa nauelewa na kujua umuhimu wa sensa ya watu na makazi ili wahamasike kushiriki zoezi hilo.


“Sensa ya watu na makazi kwa upande wa Watu wenye Ulemavu Tanzania Bara na Zanzibar tukishirikiana na Tume ya Takwimu tumeboresha huongozo wa uboreshaji wa Makarani wa Sensa kwenye Dodoso la Jamii,Kaya na Majengo pamoja na maelezo yaliyojitosheleza kuhusiana na Walemavu,” alibainisha.

MWISHO

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages