Breaking

Tuesday, 21 June 2022

SIKU YA USHIRIKA KUADHIMISHWA KITAIFA MKOANI TABORA

Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian akiaongea na wadau wa ushirika mkoani Tabora 

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Vya Ushirika Nchini Charles Gishuri alipongeza Kamati ya Maandalizi na Uongozi wa Mkoa huo kwa kazi nzuri ya maandalizi ya Maadhimisho hayo na kuongeza kuwa kila kitu kitaenda kama kilivyopagwa.
viongozi mbalimbali wakiwemo kamati ya ulinzi ya usalama ya mkoa wa Tabora wakimsikiliza mkuu wa mkoa huo.

*************

Na Lucas Raphael,Tabora


WAKULIMA, vyama vya ushirika na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo hapa nchini wametakiwa kuchangamkia maadhimisho ya siku ya ushirika duniani yatakayofanyika kitaifa katika uwanja wa Nane Nane Ipuli, Mkoani Tabora kuanzia Juni 28- Julai 2 mwaka huu ili kunufaika na fursa zilizopo.

Wito huo umetolewa jana Jumatatu Juni 20, 2022 na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake ambapo alibainisha kuwa maadhimisho hayo yatafanyika mwaka huu na mwakani Mkoani humo.

Alisema maadhimisho hayo ni fursa muhimu sana kwa wakulima, vyama vya msingi, vyama vikuu vya Ushirika, taasisi za fedha, makampuni yanayojihusisha na ununuzi wa mazao ya wakulima na wadau wote wa sekta ya kilimo nchini kuonesha shughuli zao.

Aliongeza kuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Ushirika Hujenga Ulimwengu’, hivyo akabainisha kuwa hii ni fursa muhimu kwa wana ushirika wote kuunganisha nguvu zao ili kufanya mambo makubwa.

Balozi Batilda alisema maadhimisho hayo yatapambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo maonesho ya vyama vya ushirika na wadau, makongamano mbalimbali, tuzo/zawadi, shindano la insha, upimaji afya, uchangiaji damu, kutoa misaada kwa jamii, burudani na michezo.

Alibainisha kuwa maadhimisho hayo yatafunguliwa na Waziri mwenye dhamana ya Kilimo Hussein Bashe na kufungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Alisisitiza kuwa katika siku 5 za maonesho hayo wadau watapata fursa ya kushuhudia mageuzi makubwa yanayofanyika katika sekta ya kilimo hapa nchini ikiwemo ufunguzi wa soko la kwanza la asali Wilayani Kaliua.

‘Maadhimisho haya ni fursa muhimu sana kwa wafanyabiashara, wakulima, vyama vya ushirika, taasisi za fedha, makampuni, wanunuzi wa mazao ya wakulima na wadau wote, naomba wananchi na wadau wote tujitokeze kwa wingi’, alisema.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Vya Ushirika Nchini Charles Gishuri alipongeza Kamati ya Maandalizi na Uongozi wa Mkoa huo kwa kazi nzuri ya maandalizi ya Maadhimisho hayo na kuongeza kuwa kila kitu kitaenda kama kilivyopagwa.

Alitoa wito kwa wadau wa ushindikaji, wanunuzi wa mazao ya wakulima, mabenki na wakulima kwa ujumla kujitokeza kwenye maadhimisho hayo ili kunufaika na fursa za masoko zitakazokuwepo.

Alisisitiza kuwa ili kuwa na ushirika imara hapa nchini wanaushirika wenyewe wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuuimarisha na kutumia vizuri fursa zilizopo aidha aliomba serikali kuweka mazingira bora ya shughuli za wakulima.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama Vya Ushirika Tanzania Alex Ndikile alisema wamejipanga vizuri ili kuhakikisha maadhimisho ya mwaka huu yanafana sana na kutoa fursa kwa wadau na wana ushirika wote wananufaika.

Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu na ukubwa wa maadhimisho hayo jumla ya sh mil 409 zinatarajiwa kutumika, hivyo akawataka wadau wote walioombwa mchango kukamilisha ahadi zao.

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages