Breaking

Monday, 20 June 2022

SHIRIKA LA COMPASSION LAPONGEZWA KWA KUWAWEZESHA VIJANA KIUCHUMI




SHIRIKA la kidini la Compassion International Tanzania limepongezwa kwa jitihada zake nzuri za kusaidia watoto na vijana walio na umri chini ya miaka 18 kiroho na kimwili ikiwemo kuwapa ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian Juni 19, 2022 katika mahafali ya kwanza ya ‘Huduma ya Mtoto na Kijana kwa watoto 73 waliokuwa wakilelewa, kusomeshwa na kupewa stadi za maisha na Shirika hilo ambao wametimiza umri wa miaka 22.

Balozi Dkt. Barilda amesema shirika hilo limebeba maono mazuri ya kusaidia watoto na vijana kwa kuwapa elimu ya kiroho na kimwili na maarifa yatakayowasaidia kuendeleza maisha yao, kujikwamua kiuchumi na kusaidia vijana wenzao.



Amesema kuwa vijana wanaoagwa wamefikia ukomo wa umri wa kulelewa na Shirika hilo wa miaka 22 na wamejengwa katika misingi ya uzalendo, uaminifu, uadilifu na kufanya kazi kwa bidii.

"Ninyi ni chachu ya maendeleo ya taifa, tumieni maarifa mliyopata kujiletea maendeleo na kwa manufaa ya jamii, onesheni uzalendo wa kweli, uaminifu, bidii ya kazi na uadilifu miongoni mwa jamii inayowazunguka" Dkt. Batilda

Balozi Dkt Batilda amelipongeza Shirika hilo kwa kuwezesha wazazi na walezi wa watoto hao kiuchumi kupitia Program Wezeshi, hili linaonesha jinsi wanavyojali jamii kwa kiasi kikubwa ikiwemo utunzaji mazingira.

Amewataka vijana hao kuwa na subira na kumtanguliza Mungu mbele katika mipango yao ili awaongoze katika kila hatua ya maisha yao na kuwaepusha na mambo yasiyofaa.

Aidha, ameongeza kuwa kauli mbiu ya Shirika hilo ya kumkomboa mtoto na kijana kutoka katika vifungo vya umaskini imekuwa na manufaa makubwa kwa vijana hao kwani wengi wao tayari wameanzisha miradi ya kiuchumi na kuajiri vijana wenzao.

Kwa upande wake Mlezi wa Shirika hilo Klasta ya Tabora, Askofu Elias Chakupewa wa Kanisa la Angalikana, Usharika wa Tabora amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu na kuinua wananchi kiuchumi.

Askofu Chakupewa ameomba serikali kuendelea kuweka mipango mizuri itakayowezesha watoto wote kupata haki yao ya msingi ya elimu na hata wale wanaoshindwa kwenda waweze kusaidiwa ili kuwaondolea ujinga.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa huo Panin Kerika aliwahakikishia kuwa wataendelea kuwasaidia ili watoto wote wanaolelewa katika vituo vya Huduma ya Mtoto (Compassion Centres) wapate haki yao kama dhamira ya serikali inavyoelekeza.

Akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mary Lema, Mkurugenzi wa Kanda ya Magharibi Godlisten Mao alisema wataendelea kusimamia ipasavyo dhamira ya shirika ya kuwakomboa watoto na vijana kutoka katika umaskini na kwa kuwapa ujuzi na maarifa ili kuwainua kimaisha.

Awali Mratibu wa Shirika katika Klasta hiyo, Emanuel Rusota alieleza kuwa Huduma ya Mtoto inatolewa katika jumla ya Vituo (makanisa) 11 ambapo jumla ya watoto 5128 wameshahudumiwa katika Mkoa huo.

Alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kupitia Huduma hiyo kuwa ni kuwezesha vijana 23 kufika Vyuo Vikuu, vijana 136 kuwezeshwa kupata elimu ya Ufundi Stadi katika vyuo vya VETA na kuanzishwa kwa vikundi 55 vya kuweka na kukopa ili kusaidia wazazi na walezi wa watoto hao.

Mwisho.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages