Breaking

Wednesday, 8 June 2022

SERIKALI YAFANYA TATHMINI MGOGORO KATI YA WANANCHI NA TAWA BONDE LA MTO KILOMBERO


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema Serikali imetuma timu ya wataalam ya Kitaifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi kwa ajili ya zoezi la kufanya tathmini kuhusu mgogoro kati ya wananchi wa maeneo yanayozunguka Bonde la mto Kilombero na Tanzania Wildlife Management Authority (TAWA).


Ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Mhe. Godwin Emmanuel Kunambi leo bungeni jijini Dodoma.


Amesema zoezi hilo linafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkoa, Wilaya na wananchi wa maeneo yanayozunguka Bonde la mto Kilombero. 


Aidha, amefafanua kuwa timu hiyo inafanya tathmini ya makazi na shughuli zenye athari kwenye uhifadhi wa vyanzo vya maji na rasilimali za wanyamapori ndani ya eneo la Pori Tengefu na Bonde la mto Kilombero. 


Kuhusu mgogoro kati ya hifadhi ya Serengeti, pori la akiba la Ikorongo na Vjiji vya jirani – Serengeti, Mhe. Masanja ameweka bayana kuwa kazi ya kufanya tathmini ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji imekamilika kwenye vijiji sita (6).


Ametaja vijiji hivyo kuwa ni Mbilikili, Gwikongo, Bisarara, Machochwe, Nyamakendo na Mbalibali na kusema kuwa zoezi linalofuata ni kuweka alama za kudumu kwenye mipaka ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. 


Kuhusu vijiji vya Robanda na Rwamchanga, amesema Serikali iliweka mpaka wa Pori la Akiba Ikorongo kwa kuwashirikisha kikamilifu wananchi wa vijiji hivyo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages