Na Lydia Lugakila, Kagera
Wakati serikali ikiahidi kuendelea kusimamia haki za watu wenye ulemavu imezielekeza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanapoagiza dawa na vifaa tiba pawepo na mafuta kinga kwa ajili ya watu wenye ualbino.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge akimwakilisha mgeni rasmi waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (OR -TAMISEMI) Mhe, Innocent Bashungwa katika maadhimisho ya siku ya uelewa kuhusu ualbino kimataifa yaliyofanyika Jumatatu Juni 13, 2022 katika uwanja wa Mayunga Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Akisoma hotuba ya waziri Bashungwa, RC Meja Jenerali Mbuge amesema ni vyema halmashauri zinapoagiza dawa na vifaa tiba wasisahau kuagiza pia mafuta kinga kwa ajili ya watu wenye ualbino ili kuwawezesha kuendelea kutunza ngozi zao.
Amesema kuwa halmashauri zinatakiwa pia kufanya utambuzi kwa watu wazima na watoto wenye ulemavu katika kila ngazi ya kijiji au Mkoa na kuwasajili kwenye orodha maalum.
Amesema serikali inaratibu na kusimamia upatikanaji wa mafuta kinga kwa ajili ya watu ualbino na kliniki za ngozi na kuwa mafuta ya ngozi yameingizwa katika mnyororo wa thamani na katika ugavi wa ununuzi wa dawa katika MSD.
Ameongeza kuwa serikali inaratibu vyema uundwaji wa kamati za watu wenye ulemavu katika mikoa yote 26 nchini, halmashauri zaidi ya 130, vijiji zaidi ya 5,034 Kati ya 12,319 mitaa zaidi 2,284 ambapo Kati ya 4,262 kamati zimeishaundwa huku baadhi zikihitaji kuendelea kupewa msukumo.
Awali katika lisala iliyosomwa na Bi Christina Silas ambaye ni afisa huduma chama cha watu wenye ualbino Tanzania ameoiomba serikali kuwapatia mikopo bila riba kutoka halmashauri ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi,upatikanaji wa mafuta kinga na uendelevu wa kliniki za ngozi.
Kwa upande wake katibu tawala Mkoa wa Kagera Profesa Faustin Kamuzora amezitaka halmashauri kuongeza uelewa kwa na kuanza kuandaa bajeti ya kuwasaidia watu wenye ualbino kupata mafuta ya kinga, huku akiimiza jamii kuondoa mila potofu ya kutaka mali kupitia viungo vya watu wenye ualbino kwani kwa kufanya hivyo ni ujinga.
Naye mratibu wa afya wa watu wenye ualbino Tanzania Mohammed Chanzi amesema kuwa mikakati waliyonayo ni kuhakikisha watu wenye ualbino hawaendi kwenye tiba bali kinga yao ni kuvaa kofia , kutumia mafuta kinga kujikinga na jua ili kuepuka ugonjwa wa saratani.