Breaking

Friday, 24 June 2022

SERIKALI NA WADAU KUBORESHA USTAWI WA MABAHARIA NCHINI

Na Lydia Lugakila, Lango La Habari


Serikali ikishirikiana na wadau wamejipanga kuboresha wa ustawi wa mabaharia nchini kwa kutatua changamoto zao.


Kauli hiyo imetolewa  na katibu mkuu ya wizara ya ujenzi, mawasiliano na uchukukuzi Zanzibar Amour Hamil Bakari kwa niaba ya waziri wa ujenzi mawasiliano na uchukukuzi Zanzibar katika ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya mabaharia iliyofanyika kitaifa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera yenye kilele chake juni 25 mwaka huu.


Amour amesema kuwa mabaharia wanafanya kazi katika mazingira hatarishi  kwani kundi kubwa la vijana halina ajira, na ni kazi yenye kukabiliana na hatari au majanga mbali mbali ikiwemo kupoteza maisha hivyo kuna haja kwa wadau mbali mbali kuhakikisha kundi hilo linatizamwa upya.


Amesema kuwa mabaharia na wavuvi ni watu wanaochangia sana katika mchakato wa ukuaji wa uchumi kitaifa na kimataifa licha ya ugumu wa kazi hiyo hivyo ni kundi  linalopaswa kuvaliwa njuga.


Amewasisitiza wadau na wasimamizi  kuzingatia  na kuweka mikakati maalum kuhakikisha kwamba vijana wanaoajiliwa wanapata ajira katika meli,mishahara mizuri, kuwa na bima ili kupatiwa fidia yanapotokea majanga.


" Niwashukuru waandaaji wa shughuli hii TASAC na serikali inatambua mchango mkubwa katika sekta ya bahari na pia inatambua changamoto zao ambapo asilimia 90 ya bidhaa ulimwenguni zinasafirishwa kwa kupitia usafiri wa majini"alisema katibu mkuu huyo.


Ameongeza kuwa mabaharia wanatakiwa kujenga ujasiri wa kueleza changamoto wanazokumbana nazo katika kazi zao kwa wadau wengine,   wamiliki na serikali wana wajibu wa kusikiliza kwa umakini na kuzifanyia kazi changamoto hizo ili kuimalisha na kuboresha ustawi wa mabaharia kwa hali ya Sasa na baadae.


Awali akisoma taarifa fupi katibu mkuu wa chama cha mabaharia Zanzibar Hussein Nassor amezitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni ukosefu wa ajira, mabaharia wanawake kukosa mazingira mazuri, kufanya kazi bila mikataba, kuwepo kima cha chini cha mshahara.


Aidha Nassor ameiomba serikali kuwasaidia mabaharia kupata ajira katika kampuni za nyumbani, kuziomba wizara na mamlaka zinazohusika kuruhusu wamiliki wa meli kutochukua wafanyakazi wasiokuwa na utaalam na ambao hawakusajiliwa katika vyama vya wafanyakazi.


Naye mkurugenzi mkuu mamlaka ya usafiri baharia Zanzibar Bi Sheikha Ahmed Mohamed amesema kuwa mabaharia wanafanya kazi ngumu na yenye hatari ambapo kila siku meli zinaungua moto, zinazama na kutekwa na waharifu, kufanya safari katika maeneo yenye vita kwa ajili ya kupeleka huduma muhimu ikiwemo madawa na chakula jambo linalosababisha mabaharia kupoteza maisha yao.


Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Mabaharia kufanyika juni 25, 2022 yakiwa yamebeba kauli mbiu " Safari yako ya sasa na baadae tushirikishe"

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages