Breaking

Sunday, 26 June 2022

SERIKALI KUPITIA TASAC WAFANYA MAKUBWA KWA MABAHARIA NCHINI


Na Lydia Lugakila, Lango La Habari 


Serikali kwa kushirikiana na shirika la uwakala wa meli Tanzania wameahidi kuendelea kuwapambania kwa nguvu zote mabaharia nchini, ili kuzalisha mabaharia waliokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.


Kauli hivyo imetolewa na katibu tawala Mkoa wa Kagera Prof.  Faustin Kamuzora mgeni rasmi kwa niaba ya waziri wa ujenzi na uchukuzi(SMT)  katika siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mayunga Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera juni 25, 2022.


Prof Kamuzora amesema kuwa serikali kupitia TASAC wameendelea kushirikiana vyema ili kuboresha mazingira ya mabaharia ambapo amesema serikali imeendelea kuwajali mabaharia kwani tayari imeamua kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 23.1, kulinda haki za mabaharia, afya, mazingira bora ya kufanyia kazi, huduma za matibabu na utaratibu wa mabaharia kuwasilisha malalamiko endapo baadhi ya vipengele vinapokiukwa ikiwemo kutatua changamoto zao.


Amesema mabaharia ni nguvu kubwa katika kukuza uchumi wa nchi hivyo wataendelea kupewa heshima kubwa kwa kazi na taaluma zao wanazopata kwa kuzingatia umuhimu wa watumishi hao wa meli.


Amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TASAC na chuo Cha bahari(DMI) wameendelea kufanya mazungumzo na kampuni moja kubwa kwa ajili ya mabaharia kupata mafunzo maalum, ambapo  TASAC imeendelea kuboresha huduma za  kutoa vyeti, ambapo wanatumia siku 3 kuhakiki cheti, kusimamia ubora wa mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika vyuo ili kufanya mmabaharia kuwa na ujuzi wenye viwango vinavyokubalika ndani na nje ya nchi.


Katibu tawala huyo ameongeza kuwa serikali kupitia TASAC wameendelea kushirikiana na wizara ya ujenzi na uchukuzi na ofisi ya takwimu ya taifa wizara ya mifugo na uvuvi kwa kufanya sensa ya vyombo vya majini nchi nzima ili kuwatambua mabaharia wadogo wadogo wanaoendesha vyombo vya majini kwa lengo la kupata fursa za mafunzo yatakayowasaidia kuwa na vyeti na kufanya kazi kwa weledi.


"Sekta ya usafiri wa majini ina fursa kubwa hivyo niwahimize wananchi Mkoani Kagera na watanzania kwa ujumla kujenga hali ya kujifunza elimu ya ubaharia na kuenzi mabaharia.




Naye Bi Josephine Bujiku kaimu Meneja masoko na uhusiano wa TASAC amewashukuru washiriki wote kutoka Tanzania bara na visiwani na wenyeji Kagera kwa maadalizi makubwa ya tukio hilo huku akitaja shughuli zilizofanyika ikiwemo zoezi la kuonyesha kwa vitendo namna ya uokoaji katika ajali au inapotokea dhoruba majini.


Pia washiriki kutoa elimu ya usalama wa usafirimajini kwa wanafunzi ikiwemo kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya fani ya ubaharia ambapo jumla ya wanafunzi 4,200 kutoka shule za sekondari Mkoani Kagera ikiwemo shule ya sekondari Rugambwa, Bukoba, Kahororo na Ihungo wamenufaika na elimu hiyo.


Bi Bujiku ameongeza kuwa elimu hiyo itaongeza hamasa kwa watanzania na wananchi Mkoani Kagera kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya usafiri majini.


Kwa upande wa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TASAC Capt. Mussa Hamza Mandia amesema mabaharia ni nguzo kubwa kiuchumi na kuwa nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya maji hivyo vitumike vyema na kuwa TASAC wanalenga kutembelea maeneo mengi zaidi ikiwemo kukagua  miundo mbinu yake na  usalama wa raia ikiwemo kutoa elimu zaidi juu ya ubaharia.


Hata hivyo Bi Amina Mohamed ambaye ni baharia ametajwa kufurahishwa na maadhimisho hayo kwani yamelifanya kundi la wanawake mabaharia kukumbukwa tofauti na kipindi cha nyuma ambapo mwanamke baharia alikuwa hawezi kupata ajira hapa nchini hadi aende nje ya nchi.


Hata hivyo maadhimisho ya mabaharia duniani huadhimishwa kila ifikapo juni 25 ya kila mwaka na kwa mwaka 2022  yamebeba kauli mbiu isemayo " SAFARI YAKO YA SASA NA BAADAE TUSHIRIKISHE.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages