Breaking

Tuesday, 28 June 2022

SERIKALI KUENDELEA KUTATUA MIGOGORO YA MIPAKA KATI YA HIFADHI NA MAKAZI YA WANANCHI


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto za migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na wananchi ili wananchi wajue maeneo ya vijiji na kuheshimu mipaka ya Hifadhi.


Ameyasema hayo leo Juni 28, 2022 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nkasi, Mhe. Aida Joseph Khenani, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupitia mipaka ya Hifadhi na Makazi ya Wananchi Wilayani Nkasi.


Amefafanua kuwa Serikali imeweka vigingi 111 kati ya 322 vinavyohitajika katika Pori la Akiba Lwafi Wilayani Nkasi ili kuainisha mipaka ya hifadhi hiyo.


Aidha, amesema Serikali inaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutambua na kuheshimu mipaka ya Hifadhi.


Kuhusu migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Vilima Vitatu, Mwada na Ngolee na Hifadhi ya Tarangire Wilayani Babati, Mhe. Masanja amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itatuma wataalam kwenda kufafanua au kutafsiri mipaka ili wananchi wajue maeneo ya vijiji na kuheshimu mipaka ya hifadhi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages