Breaking

Friday, 10 June 2022

RAIS SAMIA ATOA MAELEKEZO KWA WIZARA YA MAJI MRADI WA MAJI KAGERA

Na Lydia Lugakila, Kagera


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa waziri wa maji, Jumaa Aweso na katibu mkuu wizara hiyo mhandisi Anthony Sanga kuhakikisha wanazikopesha mamlaka za maji Mkoani Kagera kiasi cha shilingi milioni 500 ili ziweze kutekeleza miundo mbinu ya maji kwa wananchi kwa haraka.


Rais Samia ametoa maelekezo hayo juni 09, 2022 wakati akizindua mradi wa maji Kyaka - Bunazi wilayani Misenyi Mkoani humo  uliogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 15.7 utakaowanufaisha wananchi 65.470 wa kata ya Kyaka - Bunazi pamoja na vitongoji vyake.


"natoa maelekezo kwa waziri wa maji na katibu mkuu naomba muwakopeshe mamlaka za maji za maeneo haya shilingi milioni 500 ili iwe nyenzo ya kuwepo maji kwa haraka Sana alisema Rais Samia.


Amewataka wananchi wilayani Misenyi kuendelea kutunza miundombinu ili huduma hiyo iwe endelevu ikiwa ni pamoja na kutofanya shughuli za aina yoyote ndani ya mto Kagera  kwani ukikauka huduma hiyo itatoweka.


Ameongeza kuwa serikali itaendelea kutekeleza miradi mbali mbali kwa wananchi ikiwemo huduma bora za maji safi pamoja na huduma nyinginezo.


Aidha Rais Samia amesema maji ni uhai na kila tone la maji lina gharama kubwa na kuomba maji yatakayotumika  yalipiwe huku akiwaonya wanaotoza bili za maji kutowabambikizia wananchi bili bali wananchi walipe  kwa jinsi wanavyotumia.


Kwa upande wake waziri wa maji Jumaa Aweso ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya Mhe Rais ambapo pia amempongeza Rais Samia kwa kuiwezesha wizara hiyo fedha iliyowasaidia  kujenga  miradi mbali ya maji yenye kujitosheleza hapa nchini


Amesema miaka ya nyuma wananchi walayani Misenyi mkoani Kagera walipoteza maisha kwa sababu ya kuliwa na mamba, kutumbukia mtoni, kutumia maji yasiyofaa.


Naye katibu mkuu wizara hiyo mhandisi Anthony Sanga amesema mradi huo una uwezo wa kuzalisha maji takribani lita milioni 8 na laki 2 wakati mahitaji ya mji wa Kyaka na Bunazi ni lita milioni 5 na laki 2 na kuwa mradi huo unatumia chanzo cha mto Kagera na ni mradi  wa kwanza mkubwa kujengwa Kati chanzo cha mto huo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages