Breaking

Friday, 10 June 2022

RAIS SAMIA AFUNGUA MSIKITI WA ISTIQAAMA BUKOBA, AWAASA WAUMINI KUSHIRIKI SENSA

 Na Lydia Lugakila, Kagera


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi hususani waumini wa dini ya kiislam  kuachana na imani potofu kuhusu zoezi la Sensa litakaloanza Agosti 23 mwaka huu kwa kuwa dini ya Kiislam imeelekeza kushiriki zoezi hilo.


Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa Juni 10, 2022 katika Hafla ya ufunguzi wa rasmi wa Msikiti wa Jami'ul ISTIQAAMA Bukoba kwa kusema hata Mtume Mohamed alikuwa akifanya sensa wakati alipokuwa anaandaa vikosi vya ulinzi na usalama.


Amesema Mtume Mohamed alikuwa akihesabu askari wake ili kujua wangapi wanaenda vitani ni wangapi wanabaki kuimarisha ulinzi nyumbani, wangapi wanabaki na silaha na kadharika.


Kwa upande wake Mufti na Shekhe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Bin Zuberi amewataka Waislam na waumini wa dini nyingine kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa kwani yapo maandiko katika vitabu vitakatifu yanayoelekeza jinsi ya kushiriki zoezi la sensa.


Amesema kumekuwepo na mashekhe ambao wamekuwa wakiwafundisha imani potofu ya kutoshiriki zoezi la sensa na kuwataka kutumia nafasi zao kuwahimiza waumini kushiriki sensa.


Pia amekemea tabia ya mauaji ambayo yamezuka kwa kiwango kikubwa nchini na kuwaomba viongozi wa dini zote nchini kuhakikisha wanaongeza jitihada za mafundisho ya kuwabadilisha wa waumani kuachana tabia ya mauji.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amewasisitiza wananchi wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kuhesabiwa katika zoezi la sensa ili kuisaidia serikali kujua idadi ya wananchi wake na kuwapangia bajeti ya maendeleo.


Hata hivyo amesema serikali haiwezi kupanga maendeleo kwa wananchi wake kama haiwajui kwa idadi.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages