Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul leo Juni 1, 2022 amewaongoza watanzania kuangalia Filamu ya Royal Tour, kushuhudia na kupiga picha na Kombe la Dunia la FIFA katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Gekul ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya kuitangaza Tanzania ya Royal Tour ambaye pia ni Katibu Mkuu wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi na watendaji wa sekta ya michezo nchini.
Akizungumza kabla ya kuanza kutazama Filamu ya Royal Tour, Mhe. Gekul amewapongeza Coca Cola kwa kudhamini ujio wa kombe hilo nchini.
Ameongeza kuwa ujio wa Kombe hilo ni ishara kuwa FIFA inathamini jitihada zinazofanywa na Serikali kwenye Michezo.
Amesema kwa sasa Serikali inakusudia kuanzisha vituo vya michezo na kurudisha Kombe la Taifa ambalo linakwenda kuibua vipaji.
Wasanii mbalimbali wakiongozwa na Sholo Mwamba wametumbuiza wakati Dkt. Abbasi pia akichana mistari na kuwashangaza wapenzi wa hip hop waliokuja kushuhudia kombe na kutazama Royal tour.