Kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha wananchi wote kuungana kupinga vitendo vya ukatili wa aina zote kwenye jamii ijulikanayo Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA), imezinduliwa rasmi katika kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika mkoani Dodoma.
Akizindua Kampeni hiyo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amebainisha kuwa, pamoja na jitihada mbalimbali za kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa watoto, bado taarifa za vitendo hivyo hususani kwa watoto zinaendelea kuongezeka ikiwemo Ubakaji, Ulawiti, Utumikishwaji wa watoto katika ajira hatarishi, Ukeketaji, Ndoa na mimba za utotoni na vitendo vingine vya ukatili.
Mhe. Dkt. Gwajima amesema licha ya watuhumiwa wa ukatili kuchukuliwa hatua kali za kisheria Takwimu za Jeshi la Polisi, zinaonesha idadi ya matukio inashamiri.
"Kulingana na takwimu za Polisi Tanzania katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2021 jumla ya matukio ya ukatili kwa watoto yaliyoripotiwa katika jeshi la Polisi ni 11,499 ikilinganishwa na matukio 15,870 katika kipindi kama hicho mwaka 2020 (upungufu ni matukio 4,371 sawa na asilimia 27.5)." amesema Mhe. Gwajima.
Waziri Gwajima ameitaja Mikoa iliyoongoza kwa vitendo hivyo ilikuwa ni Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489). Aidha, makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji (5,899), mimba kwa wanafunzi (1,677) na ulawiti (1,114). Kwa upande mwingine, utafiti wa serikali na UNICEF unaonesha asilimia 60 ya matukio yanatokea nyumbani na asilimia 40 yanatokea mashuleni.
Waziri Gwajima ameongeza kuwa, kampeni hiyo ya SMAUJATA ni shirikishi kwa lengo la kuongeza nguvu na kasi ya kupambana kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto na kwenye jamii kwa ujumla.
"Wizara kwa kushirikiana na wadau wake zikiwemo Wizara mbalimbali za kisekta tunaratibu kampeni shirikishi ya jamii inayoenda kwa jina la SMAUJATA (Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, 2022). Dhana ya Kampeni hii ni kuandikisha wanachama wengi zaidi kutoka ngazi zote na mitandao yote ya jamii wanaokerwa na uwepo wa ukatili, wenye moyo wa kujitoa bila ujira wowote kwenye kuelimisha jamii ili ifahamu juu ya uwepo wa ukatili na athari za ukatili na hatua gani wachukue kabla ya ukatili kufanyika na pale ambapo umefanyika". amesema mhe. Gwajima.
Amebainisha kwamba Kampeni hiyo imepokelewa kwa mtazamo chanya mpaka sasa wananchi zaidi ya 5000 wameshajiunga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampeni ya SMAUJATA Sospeter Bulugu amesema yeye pamoja na vijana wenzake wazalendo wamejitolea kushirikiana na Serikali katika kupambana na vitendo vya ukatili hasa kwa Watoto ndani ya jamii yote.
"Tulipokuwa jeshini tulifundishwa kuhusu uzalendo, tuliambiwa uzalendo ni kuipenda nchi yako pamoja na kuitumikia kwa mambo yatakayoleta mabadiliko kwenye jamii yako, kwetu kama SMAUJATA, kupokelewa na Serrikali kufungua Milango ni ishara kwamba tutatiza ndoto zetu za kuisadia Jamii na kuwa na Jamii huru" amesema Bulugu.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Stanslaus Nyongo akizungumza na watoto pamoja na hadhara iliyoshiriki maadhimisho hayo amesema kwa sasa malezi ya watoto yanahitaji msukumo tofauti na malezi ya miaka ya nyuma kwa sababu Dunia imebadilika.
"Mhe Mgeni Rasmi na ndugu waalikwa Naomba nimuhakikishie Mgeni Rasmi na wananchi wote kuwa nikiwa Mwenyekiti wa Kamati pamoja na wanakamati wenzangu tutasimama kidete kutetea Ajenda yoyote inayohusu kupinga ukatili ndani ya Jamii ikiwemo kuishauri na kuisimamia Serikali katika usimamizi wa sheria zinazowalinda watoto" amesisitiza Mhe. Nyongo.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika nchini yamefanyika kwenye ngazi za Mikoa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum iliuungana na Mkoa wa Dodoma katika Viwanja vya Nyerere Square.