Na Lydia Lugakila, Kagera
Jumuiya ya wafanyabiashara Mkoa wa Kagera wameazimia kutoa hati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutokana na kusamehewa madeni ya tozo na Kodi mbali mbali.
Kauli hiyo imetolewa juni 13, 2022 na Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara Mkoa wa Kagera, Nicholaus Jovin walipokutana na waandishi wa habari katika hoteli ya victorious iliyopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Jovin amesema kuwa hatua hiyo ya furaha kwa wafanyabiashara hao imekuja kutokana na kauli ya Rais Samia aliyoitoa hivi karibuni akiwa Mkoani Kagera katika ziara ya siku 3 ambapo alitoa msamaha wa kodi iliyokuwa imelimbikizwa kwa muda mrefu.
"Sisi kama wafanyabiashara wa Mkoa huu tunaipongeza serikali ya awamu ya sita kupitia Rais Samia kwakweli kauli yake imechochea muitikio kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zetu bila wasi wasi kwani kipindi cha nyuma tulikumbana na changamoto nyingi" alisema mwenyekiti wa jumuiya hiyo.
Aidha ameongeza kuwa wanaahidi kushirikiana bega kwa bega na kufanya mabadiliko yatakayofanya Mkoa huo unaondokana na tatizo la kuwa nyuma kiuchumi.
Kwa upande wao wajumbe wa jumuiya hiyo akiwemo Richard Maganga wamesema kauli ya Rais hakika imewapa nguvu za kupambana kiuchumi.
Mwisho