Na Mwandishi Wetu, Mara
Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo EMEDO limeutambulisha rasimi mradi wa kuzuia ajali za kuzama majini Kwa wadau Wa Uvuvi wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza leo Ijumaa Juni 10, 2022 na Wadau hao wa Uvuvi Mratibu wa Mradi huo kutoka EMEDO Arthur Mugema amesema kabla ya kuanza Kwa mradi huo utafiti ulifanyika Ili kujua ukubwa wa tatizo hilo Kwa Ziwa Victoria.
Mugema amesema katika utafiti walioufanya waligundua sababu mbalimbali zinazochangia ajali za majini.
Amezitaja Moja ya sababu kuwa ni matumizi ya pombe,ubebaji wa mizigo mikubwa,kuto kuvaa majaketi ya kuzuia kuzama na mitumbwi Kutokuwa na taa nyakati za usiku.
Kwa upande wake Victor Bernard afisa takwimu wilaya ya Musoma amesema Bado Kuna tatizo kubwa la kupata takwimu halisi za ajali za majini kutokana na mfumo uliopo.
Bernard amesema takwimu nyingi zinazopatikana ni takwimu za mazao ya ziwani na idadi ya wananchi wanaojishughulisha na Uvuvi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa EMEDO Editrudith Lukanga amesema tayari mradi wa kuzuia ajali za kuzama majini umeanza na utadumu Kwa miaka mitatu ambapo elimu imeanza kutolewa Kwa Jamii ya Wavuvi waishio pembezoni mwa Ziwa Kwa ushirikiano mkubwa na Serikali.