Na Mwandishi Wetu, Sengerema
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemtaka Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha kukamilisha kwa wakati uthaminishaji wa maeneo ya wananchi yaliyochukuliwa na mgodi wa Sotta Mining Limited uliopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza ili waanze kulipwa gharama za maeneo yao.
Dkt. Kiruswa ametoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara katika mgodi huo unaomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali yenye hisa za asilimia 16 na Kampuni ya Orecop Tanzania Limited yenye hisa za asilimia 84.
Amesema kati ya watu 1,606 wanaoishi kuzunguka eneo la mgodi watu 1,455 wamefanyiwa uthaminishaji, watu 1239 sawa na asilimia 85 waliochukua Fomu Namba 3 ya kukubali kulipwa na watu 216 sawa na asilimia 15 wamekataa kuchukua fomu za malipo.
Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa kuna baadhi ya watu wameendeleza maeneo aidha kwa kujenga nyumba, kupanda mazao na miti katika maeneo mbalimbali baada ya kikomo cha kuendeleza maeneo yanayotegemewa kuchukuliwa na mgodi ya Nyanzaga Mining Limited.
Sambamba na hayo, Dkt. kiruswa amesema kati ya watu 1,606 wanaoishi kuzunguka eneo la mgodi watu 1,455 wamefanyiwa uthaminishaji, watu 1239 sawa na asilimia 85 waliochukua fomu namba 3 ya kukubali kulipwa na watu 216 sawa na asilimia 15 wamekataa kuchukua fomu za malipo.
Dkt. Kiruswa amesema kuna Haki ya Ardhi na Haki Madini ambapo Wizara ya Madini inasimamia Haki ya Madini na Wizara ya Ardhi inasimamia Haki ya Ardhi na kuongeza kuwa, kazi ya Wizara ya Madini ni kutoa leseni za uchimbaji, kusimamia usalama maeneo ya uchimbaji pamoja na kusimamia mpango wa ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika Sekta ya Madini.
Dkt. Kiruswa amesema, ajira zitakazotolewa katika mgodi huo, watu watakaopewa kipaumbele ni wanakijiji wanaoishi katika eneo linalozunguka mgodi huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amesema Serikali kupitia Mtathmini Mkuu wa Serikali alifanya tathmini na kubaini maeneo yanayozunguka mgodi wa Nyanzaga Mining Limited yanathamani ya shilingi milioni mbili kwa heka moja.
Pia, Waziri Mabula amesema mgodi utalipa mazao yaliopo katika eneo husika, nyumba, makaburi, posho ya usafiri kwa tani 12 kwa kilometa 20 na posho ya miezi 36 kwa ajili ya kuanzia maisha.
Ameeleza kuwa, baadhi ya wananchi wanaoishi katika eneo linalozunguka mgodi wa Nyanzaga Mining Limited hawana elimu ya kutosha kuhusu faida watakazozipata baada ya mgodi kuanzia uzalishaji ambapo amewataka watendaji wake kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hao.