Na Said Muhibu, Lango La Habari
Klabu ya Chelsea imeonesha nia ya kumsajili mchezaji wa Manchester City Raheem Sterling huku mshambuliaji wake Romelu Lukaku akitarajiwa kurejea Inter Milan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la The Sun limeripoti winga huyo matata mwenye umri wa miaka 27 amebakiza mwaka mmoja kusalia kwenye timu yake na amehusishwa katika orodha ya wachezaji ambao Chelsea inawawania kwa msimu ujao.
Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel amekuwa ni shabiki mkubwa wa Sterling na anavutiwa sana kumsajili katika timu yake ili kuimarisha zaidi safu yake ya ushambuliaji.
Sterling mwenye magoli 131 katika michezo 339 aliyocheza akiwa Manchester City anatarajiwa kuondoka klabuni hapo kama mchezaji huru msimu ujao, ijapokuwa Manchester City inahitaji kumuuza kwenye dirisha kubwa la msimu huu kwa kiasi cha £60 milioni.
Kwa upande wake Romelu Lukaku amehusishwa na kurejea timu yake ya awali Inter Milan kwa msimu ujao, baada ya kuwa na msimu mbaya tangu asajiliwe na klabu ya Chelsea kwa kiasi cha £97.5 milioni katika kipindi cha majira ya joto.
Aidha, Chelsea ipo mbioni kumsajili mchezaji wa Barcelona Ousmane Dembele mwenye umri wa miaka 25 ambaye bado hajapata muelekeo wa malengo yake na klabu aliyopo hivi sasa.