Na Lango La Habari
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imesaini makubaliano ya ushirikiano na Tume ya ushindani (FCC), wakati huo huo FCC ikisaini na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), yenye lengo la kuboresha mazingira uwekezaji nchini.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema BRELA ipo tayari kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mbalimbali pale zinapohitajika.
Bw. Nyaisa amesema kuwa ushirikiano wa taasisi hizo za Serikali ambazo zinawezesha biashara utatoa fursa kwa wawekezaji kupata masoko ya uhakika huku bidhaa zao zikiwa zinatambulika na Mamlaka husika.
"Ndugu wanahabari tunaomba muufahamishe Umma wa Watanzania na wawekezaji kuwa utiaji saini huu unalenga kufungua milango zaidi ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuondoa migongano ya hapa na pale ambayo inaweza kuchelewesha michakato ya urasimishaji wa biashara, hivyo tunafanya haya kuhakikisha wawekezaji wanakamilisha michakato ya ufanyaji Biashara kwa wakati," amefafanua Bw. Nyaisa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bw. William Erio amesema yanapotokea malalamiko ya mtu kutumia alama ya biashara ya mwingine FCC huomba taarifa kutoka BRELA kwani ndiyo yenye dhamana ya kusajili majina ya biashara, kampuni na alama za biashara.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji amesema SIDO kama mlezi wa viwanda vidogo itahakikisha inatoa ushauri na kuhimiza wadau wanaopata mafunzo kurasimisha biashara zao BRELA, ili kukidhi vigezo katika soko la ndani na nje ya nchi.
Utiaji saini makubaliano hayo yamefanyika tarehe 23 Juni, 2022 katika ofisi za FCC, Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, yanayozitaka Taasisi chini ya Wizara hiyo, kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuvutia wawekezaji na kufanya Tanzania kuendelea kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI