Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imewaachia huru washtakiwa wote saba ambao ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, baada ya mahakama hiyo kusema kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri kugubikwa na utata.
Sabaya na wenzake, walikuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 27 ambapo wameachiwa kwa kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na mapungufu ya kisheria.
Mbali na Sabaya wengine ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.
Hata hivyo Sabaya, Nyegu, Aweyo na Msuya wataendelea kubaki mahabusu katika gereza la Karanga kwa kuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.
Hii ni kesi ya pili Sabaya kushinda ambapo Mei 6, 2022 na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, walishinda rufaa iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, waliyokata kupinga hukumu ya miaka 30 iliyokuwa imetolewa na na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.