Breaking

Thursday, 16 June 2022

BALOZI POLEPOLE AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO NA KUTETA NA RAIS WA MALAWI + Video



Lilongwe, Malawi

Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Humphrey Polepole amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Malawi Dkt. Lazarus Chakwera pamoja na kufanya mazungumzo ya kuimarisha uhusiano.

Balozi Polepole amewasilisha utambulisho huo leo Alhamisi Juni 16, 2022 katika Kasri la Kamuzu, Jijini Lilongwe pamoja na kuzungumza faragha na Rais Chakwera ambapo ametumia fursa hiyo kumfikishia salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Balozi Polepole amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia inaendelea kuthamini mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Nchi hizo ambapo Tanzania iko tayari kuihudumia Nchi ya Malawi katika Ushoroba wa Mtwara na kuwa imekamilisha ujenzi wa zaidi ya kilometa 800 za barabara ya lami kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na kuweka meli tatu kubwa katika Ziwa Nyasa.

“Serikali imeweka Meli tatu kubwa katika ziwa Nyasa, mbili zikiwa za Mizigo na zenye uwezo wa kubeba Tani 1,000 na Meli ya Abiria yenye uwezo wa kubeba zaidi ya Abiria 100 na Mizigo Tani 200 na ziko tayari kuanza kutoa huduma katika upande wa Malawi.” Amesema Balozi Polepole

Aidha Balozi Polepole ameongeza kuwa Seikali ya Tanzania inafuatilia kwa karibu hatua anazozichukua Rais Chakwera katika kufanya Mageuzi ya Kiuchumi na kijamii pamoja na jitihada zake za kufanya marekebisho na maboresho ya Taasisi za Umma ili ziweze kuwa madhubuti katika kuwahudumia wananchi wa Malawi.

“Kazi hiyo sio rahisi na inataka kujitoa ili kufikia maono yake ya kuwa na uchumi imara na jumuishi na hatimaye nchi ya kipato cha kati kama ilivyo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa la Malawi ya Mwaka 2063, Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inamuunga mkono katikajitihada hizo” Amesema Balozi Polepole.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Malawi Lazarus Chakwera ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia Malawi sehemu ya Bandari ya Dar Es Salaam na Bandari kavu ya Mbeya na ameelezea umuhimu wa kuhuisha matumizi wa Ushoroba wa Mtwara.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages