Mwanaume mmoja Mkazi wa Kitongoji cha Lubela, Mtaa wa Nyashimbi, Kata ya Mhongolo wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Bundala Mathew anashikiliwa na Polisi, kwa tuhuma ya kumuua mkewe, Rehema Nyamgila kwa kumcharanga mapanga.
Imedaiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, alitenganisha viungo vya mwili wa mkewe na kuchukua baiskeli na kuvisafirisha mpaka mbugani usiku wa manane na kuvitawanya ili kupoteza ushahidi.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, Magdalena Katambi ambaye ni mtu wa karibu na familia hiyo, alidai kuwa tukio hilo liligunduliwa na mtoto wa marehemu, Ezekiel Bundala tarehe 27 Mei 2022.
"Nilienda kumjulia hali mtoto aliyekuwa anaumwa, ndipo Ezekia akanijulisha kuwa mama yake hayupo funiani.
“Ameniambia aligombana na baba yake kwa kuwa aliona beseni likiwa na damu lakini baba yake akawa anasema hizo ni rangi tu na siyo damu.”
Anasema wakatoa taarifa kwa ndugu, majirani na Polisi, ndipo mtuhumiwa baada ya kubanwa akawapeleka alipoutupa mwili, wakaukuta ukiwa umekatwa vipande.
Alidai ljumaa mwili ulipelekwa kuhifadhiwa mochwari ya Hospitali ya Manispaa ya Kahamana, 28 Mei 2022, Polisi walirudi na mtuhumiwa kuonesha mahali alipohifadhi viungo vingine vya mwili huo, ndipo kichwa kikapatikana kimezikwa juu ya kaburi la marehemu babu yake kwa mama.
Magdalena alidai viungo vingine vya sehemu za siri na matiti vilipatikana karibu na mlango, kwenye mafiga ya jiko, ndipo alipozika, huku akitaka watoto wake wapikie hapo mara kwa mara, kwani ameweka mbayuwayu wake akauke kwa ajili ya kutengenezea dawa.
"Baada ya askari kumhoji tena wapi vilipo viungo vingine, aliwapeleka mbugani ulikookotwa mwili katikati ya majaruba ya mpunga ilipatikana mikono na magoti, lakini wakati huo vidole vya mikono na miguu havikuonekana, kwa kweli tukio hili limetusikitisha na kutuachia simanzi kubwa," alisema Magdalena.
Hata hivyo, mama mzazi wa mtuhumiwa, Mhoja Bundala alidai kupata taarifa kwa watu kuwa mwanawe ameachana na mkamwana wake, hivyo akawa anasubiri taarifa rasmi kutoka kwake, lakini ajabu aliletewa taarifa za tukio hilo la kushitua.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyashimbi, Peter Nzingula alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Mei 27, 2022.
Anasema alipohojiwa chanzo cha kufanya unyama huo, mtuhumiwa alidai alikuwa na wivu wa mapenzi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mhongolo, Boniphace Maziku alidai kuwa tukio hilo lilitokea kwenye kata yake Mtaa wa Nyashimbi, na alishirikiana na viongozi wa ngazi ya mtaa, kutoa taarifa sehemu husika, na sasa uchunguzi wa tukio unaendelea Polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, George Kyando amethibitisha uwepo wa tukio hilo na kuongeza kuwa uchunguzi wake unaendelea, na sheria itachukua mkondo wake.
Marehemu Rehema ameacha watoto wanne.