Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia Warren Mwinuka (20) Mkazi wa Mtaa wa Makondeko jijini Mbeya kwa tuhuma za kujifanya ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (Juma Homera ) na kutumia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Instagram kwa jina la Mkuu huyo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema Mtuhumiwa huo alikamatwa Juni 7, 2022 majira ya saa nane mchana katika maeneo ya Mama John jijini Mbeya alipokuwa akiendelea kuwatapeli Watu.
Mtuhumiwa alikuwa akitumia akaunti hiyo kuwahadaa Watu kwa kujifanya ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na kutoa namba ya simu yake ili Wananchi waweze kutoa na kumfikishia kero au shida mbalimbali na alitumia fursa hiyo kutapeli.
Kwa upande wake Mtuhumiwa amejitetea kuwa sababu ambayo ilimpelekea hadi kufanya hivyo ni kwakuwa anampenda sana Mkuu wa Mkoa huyo lakini Polisi wamesema upelelezi wa shauri hilo unaendelea na ukikamilika Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani.