Breaking

Sunday, 5 June 2022

AJALI YA MOTO YAUA WATU 40 HUKU ZAIDI YA 200 WAKIJERUHIWA - BANGLADESH


Vifo vilivyotokana na ajali ya Moto mkubwa uliozuka katika ghala la kuhifadhia makontena Sitakunda, kusini mashariki Nchini Bangladesh, vimezidi kuongezeka na kufikia watu 40 huku majeruhi wakifikia zaidi ya 200.

Moto huo umezuka usiku wa kuamkia leo Jumapili Juni 05, 2022 ambapo Mamia ya watu wakiwemo wazima moto walifika kukabiliana na moto huo wakati makontena kadhaa yalilipuka katika eneo la Sitakunda.

Chanzo cha moto huo hakijajulikana, lakini inadhaniwa kemikali zilihifadhiwa katika baadhi ya makontena hayo.

Daktari Mkuu wa hospitali ya Chittagong, Elias Chowdhury amesema idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na baadhi ya majeruhi kuwa katika hali mbaya na zimeomba kuchangia damu.

Wengi wa waliojeruhiwa wanaripotiwa kuwa katika hali mbaya huku majeraha ya moto yakichukua asilimia 60 hadi 90 ya miili yao.

"Mlipuko huo ulinirusha umbali wa mita 10 kutoka mahali nilipokuwa nimesimama. Mikono na miguu yangu imeungua," dereva wa lori Tofael Ahmed aliambia shirika la habari la AFP.


Mhudumu mwingine wa kujitolea aliambia shirika hilo kuwa ameona miili zaidi ndani ya eneo lililoathiriwa na moto huo.

Takriban wazima moto watano waliuawa katika mlipuko huo na wengine kadhaa kujeruhiwa. Watu wengi bado hawajulikani walipo, wakiwemo waandishi wa habari kadhaa waliokuwa wakiripoti moto huo kabla ya mlipuko huo.

Kulingana na afisa wa serikali ya eneo hilo amesema kuwa Ghala hilo ilikuwa na mamilioni ya dola ya nguo zilizokuwa zikisubiri kusafirishwa kwa wauzaji reja reja wa Magharibi.

Inasemekana kuwa mlipuko huo ulivunja madirisha ya majengo kadhaa karibu na ulionekana kutoka maeneo ya umbali wa kilomita 4, kulingana na chombo cha habari cha Prothomalo.

Moto ulikuwa bado unawaka Jumapili asubuhi, saa kadhaa baada ya mlipuko huo. Jeshi limetumwa kuzuia kemikali zinazoingia baharini.

Mji huo uko kilomita 40 pekee kutoka mji wa pili kwa ukubwa nchini, Chittagong, na hospitali moja ya jiji hilo imefurika na wahasiriwa. Waliojeruhiwa ni pamoja na wafanyikazi wa bohari pamoja na wazima moto na polisi, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

Jeshi la zima moto bado wanahangaika kuzima moto huo leo, huku milipuko ikiendelea kuifanya kuwa ngumu zaidi, kulingana na maafisa wa zima moto.

"Bado hatukuweza kudhibiti moto kwa sababu ya kuwepo kwa kemikali hii," Main Uddin, mkuu wa huduma ya zima moto Bangladesh.

Jeshi limetumwa kuzuia kemikali zinazoingia baharini.

Ajali za moto zimezidi kuikumba nchi ya Bangladesh ambapo Mwaka jana, takriban watu 39 waliuawa baada ya feri kushika moto kusini mwa nchi. Na mapema mwaka huo huo, takriban watu 52 walikufa kutokana na moto wa kiwanda huko Rupganj karibu na mji mkuu, Dhaka.

Wafanyikazi watatu pia waliuawa mnamo 2020 baada ya tanki la mafuta kulipuka katika ghala jingine la kuhifadhia kontena huko Patenga, sio mbali na Chittagong.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages