Breaking

Tuesday, 28 June 2022

AGIZO LA WAZIRI MKUU KWA MAMEYA NA WENYEVITI WA HALMASHAURI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri wasimamie ipasavyo matumizi ya fedha zilizokusanywa na zile zinazotoka Serikali Kuu na wahakikishe zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

 

Ameyasema hayo leo Jumanne, Juni 28, 2022 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri wa Tanzania Bara katika ukumbi wa Mabeyo Complex jijini Dodoma. Amesema lazima viongozi wajue fedha zinazoingia na maelekezo yake.

 

Amesema Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kila mwaka inaibua makosa yale yale ikiwamo kuhamisha fedha kutoka fungu moja kwenda jingine bila kufuata taratibu zilizowekwa na  kufanyika kwa malipo bila ya kuwepo maelezo au vielelezo.

 

“Fedha za makusanyo kutumika kabla ya kupelekwa benki. Lazima muhoji kwa nini na mjue hilo haraka. Pia mjiridhishe pale wanaposema hakuna mtandao je ni kweli hakukuwa na mtandao. Fuatilieni na ununuzi wa vifaa hewa hasa kipindi hiki cha ujenzi wa miradi.”

 

“Viongozi wote mlioshiriki mafunzo mkasimamie vema utawala bora na utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro sambamba na ushirikishaji wananchi katika maamuzi na mipango ya maendeleo.”


Majaliwa amesema viongozi wote wanatakiwa wahakikishe wananchi wanapata taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti za kutekeleza mipango hiyo. “Utoaji wa taarifa za mapato na matumizi ni muhimu katika kujenga imani kwa wananchi.”


Waziri Mkuu amewataka viongozi hao waimarishe usimamizi wa miradi ya maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kazi zinazofanywa zilingane na fedha inayotumika. “Kasimamieni viwango vya ubora wa miradi inayotekelezwa na utekelezaji wa makubaliano yaliopo kwenye mikataba.”

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages