Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa akipokea tuzo maalum ya Wizara ya Madini iliyotolewa na CHAMMATA kwa usimamizi mzuri katika Sekta ya Madini
Tuzo ya Wizara ya Madini
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akizungumza wakati akizindua Katiba na Kanuni na kukabishi vyeti vya uanachama wa mikoa ya kimadini kwa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA) Mkoani Arusha
Mwenyekiti wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA) Jeremiah Kituyo akizungumza jambo wakati wa uzinduzi wa Katiba na Kanuni na kukabishi vyeti vya uanachama wa mikoa ya kimadini kwa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA) Mkoani Arusha
Baadhi ya Wafanyabiashara wadogo wa madini (CHAMMATA) wakiwa kwenye kikao cha Naibu Waziri wa Madini
*********
WIZARA ya Madini imetunukiwa tuzo ya heshima kwa usimamizi na utendaji bora kama kumbukumbu maalumu kwa wizara kwa kujali na kuthamini wafanyabiashara wadogo wa madini katika Sekta ya Madini.
Tuzo hiyo imepokelewa leo Mei 20,2022 na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa wakati wa kikao chake na Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA) kilichofanyika jijini Arusha.
Mwenyekiti wa Chama hicho, Jeremiah Kituyo amesema, wizara imekuwa na mchango mkubwa kwa wafanyabiashara na wachimbaji wa madini nchini.
"Tunapenda Serikali itambue kuwa CHAMMATA tunataka kuona Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa ili Tanzania inufaike ipasavyo na rasilimali ya madini nchini," amesema.
Pia, amesema CHAMMATA imetoa cheti cha pongezi kwa broka wa mkoa wa Geita, Athanas Charles ambaye ameongoza kwa ulipaji wa kodi na cheti kwa mkoa wa Arusha kwa kupokea na kukarimu ugeni wa Mabroka Kitaifa.
Amesema, chama kipo kwa ajili ya kuhamasisha wanachama wake kujishughulisha na biashara za madini aina zote kama vile Vito, madini ujenzi, Dhahabu na madini ya viwandani.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili, ameomba CHAMMATA kuanza kushirikishwa kwenye baadhi ya maamuzi ya utungaji wa kanuni au marekebisho, mapendekezo na mwongozo wa masoko.
"Lengo la CHAMMATA ni kufungamanisha, kusimamia na kuwatetea wafanyabiashara wa madini (MABROKA) nchini. Pia kuwaunganisha wafanyabiashara na Serikali, ili kukuza ustawi wa biashara ya madini nchini, kutetea na kusimamia haki za Mwanachama kushirikiana na Serikali.
"Pia, kudhibiti utoroshaji wa madini nchini, kutatua migogogro inayohusu biashara ya madini, kupata mikopo yenye riba nafuu ya kuendesha shughuli za ununuzi na uuzaji wa madini kwa wanachama na kushiriki katika maonyesho yote ya madini ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya wanachama wote,"amesema Kituyo.
Akipokea Cheti hicho, Naibu Waziri Dkt. Steven Kiruswa ameipongeza CHAMMATA kwa kutoa tuzo maalumu kwa wizara. Aidha ametoa pongezi kwa mfanyabiashara mdogo kutoka Geita, Bw. Athanas Charles kwa kupewa cheti cha pongezi kwa kutambuliwa na mamlaka ya mapato kama mlipaji mzuri wa kodi ya Serikali.
Naibu Waziri amesema, Wizara ya Madini itaendelea kutekeleza majukumu yote kwa kushirikiana na Wadau katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na matokeo chanya.
Kuhusu mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, amesema sekta ya Madini ni nguzo ya uchumi Kwa kuwa inafungamanisha Sekta nyingine katika kuleta maendeleo.
"Sekta ya Madini ni Sekta yenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu kwa kuwa ina ajiri watu wengi kupitia shughuli mbalimbali zinazoambatana katika biashara ya madini kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani, masoko na biashara ya madini," amesema Dkt. Kiruswa.
Vile vile amesema, Serikali ipo tayari kuwasikiliza na kupokea maoni ya wafanyabiashara pamoja na wachimbaji na kuyafanyia kazi.
"Naomba kuwaasa wafanyabiashara wote kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na Kanuni, kuachana na vitendo vya utoroshaji wa madini na kuwa wazalendo wa kweli katika kusimamia maendeleo ya nchi yetu yanayotokana na Sekta ya Madini," amesisitiza.
Wakati huo huo, Naibu Waziri, Dkt.Kiruswa amezindua Katiba na Kanuni za CHAMMATA.