Na Samir Salum,Lango la habari
Wizara ya madini kupitia Tume yake imeahidi kuendelea kutoa kipaumbele kwa huduma na bidhaa zinazotolewa na Watanzania kupitia Sekta ya madini.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Mei 22, 2022 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Adolf Ndunguru wakati akifunga Jukwaa la kwanza la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya madini liliofanyika Jijini Mwanza kuanzia Mei 20-22, 2022.
Ndunguru amesema kuwa Wizara kupita Tume ya Madini itaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa vipaumbele vinatolewa kwa huduma na bidhaa z makampuni watanzania katika sekta ya madini.
“lengo kuu la wasimamizi wa ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya madini ni kuhakikisha kuwa kipaumbele kinatolewa kwa huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazotolewa na Watanzania wenyewe" amesitiza Ndunguru
Ameongeza kuwa Serikali itafanyia kazi changamoto na mapendekezo yote yaliyobainishwa katika jukwaa hilo katika kuboresha sheria kanuni pamoja na miongozo ili kutengeneza mazingira rafiki ya uwezeshaji katika kuwashirikisha watanzania.
Aidha Ndunguru ametoa wito kwa washiriki wa jukwaa kufanyia kazi changamoto walizonazo na kuzingatia maazimio yaliyotolewa.
Pia amewaasa wadau wote wa sekta ya madini kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika August 23, 2022 ili kuisaidia serikali kupamba vyema mipango ya maendeleo ya nchi.
Awali katibu mtendaji wa tume ya madini Mhandisi Yahya Samamba ameelezea maazimio yaliyotolewa katika jukwaa hilo ambapo Wizara na Tume ya Madini zimetakiwa kufanya marekebisho ya sheria na kanuni katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa mbadala wa kufanya ubia na mtu binafsi badala ya kampuni, kutokuwa na ulazima wa kuomba idhini ya manunuzi katika kila hatua.
Maazimio mengine ni pamoja na Tume ya Madini kuwahimiza wamiliki wa leseni za madini kutoa mrejesho kwa watoa huduma wote wanaoshiriki zabuni na kuwaeleza mapungufu wale ambao hawakufanikiwa kupata ili waweze kufanya maboresho.
Nne, Tume ya Madini kuangalia namna boravkwa kuhusisha benki katika kuwawezesha watoa huduma kupata mikopo ya biashara bila kuwa na masharti magumu.
Pia kuandaa jukwaa la ushirikishwaji wa Watanzania walau mara mbili kwa kila mwaka na kuhusisha Taasisi za elimu ambazo zinahusika katika kufanikisha utekelezaji wa sheria na kanuni za ushirikishwaji wa Watanzania.
Jukwaa la Kwanza la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya madini lililoambatana na maonesho limefikia tamati leo Mei 22, 2022 ambapo pia Katibu Mkuu alitoa Tuzo na Vyeti kwa Wadhamini ambao ni Equity Bank (Tanzania) Limited, CMS (Tanzania) Limited, Twiga Minerals Corporation Limited na BR Drilling Limited.
Wengine ni pamoja na Tansec Limited, Boart Longyear (Tanzania) Limited, Geita Gold Mining Limited, Williamson Diamonds Limited, Tembo Nickel Corporation Limited, BG Umoja Services Limited, Epsom Limited, African Assay Laboratories, Tanga Cement Limited, Shanta Mining Co. Limited na SGA Guards Tanzania Limited.
Mwisho