Breaking

Saturday, 7 May 2022

WAZIRI MKUU AITAKA WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI KUCHUNGUZA MASLAHI YA WAFANYAKAZI DARAJA LA JPM KIGONGO BUSISI




Na Samir Salum, Lango la habari

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kukutana na wataalam wa idara ya kazi ya mkoa wa Mwanza ili kuchunguza kama kuna madai ya mishahara kwa wafanyakazi katika mradi wa ujenzi wa daraja la JPM Kigongo Busisi.


Majaliwa ametoa agizo hilo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo leo Jumamosi Mei 07, 2022 na kupokea malalamiko kutoka kwa mbunge wa Sengerema, Hamisi Tabasamu aliyedai kuwa licha ya mradi huo kuendelea lakini watumishi wamepungua na wanakimbilia katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutokana na kutolipwa stahiki zao kwa wakati.



Naye Mhandisi Mshauri wa mradi huo Mhandisi Benjamin Michael alisema awali kulikuwa na wafanyakazi 813 na sasa wamebaki 744 baada ya wengine kuacha kazi.


Kutokana na hilo Waziri mkuu ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na watendaji wa Idara ya Kazi mkoa wa Mwanza kuhakikisha watumishi katika mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi wanalipya stahiki zao ipasavyo.


Aidha amemuagiza Mkandarasi anayejenga daraja hilo kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi kwa wakati.


Baada ya ukaguzi huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakagua Ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema pamoja na kuzungumza na watumishi na wananchi wa Halmashauri hiyo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages