Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa usiku wa leo majira ya saa nne usiku , Mei 28, 2022 amewaongoza mamia ya wapenzi wa soka nchini kutazama mbashara fainali za mashindano ya 67 ya UEFA baina ya Timu ya Real Madrid na Liverpool kupitia DStv kwenye daraja jipya la Tanzanite jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mchengerwa ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu, Saidi Yakubu na Watendaji kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Kabla ya mechi hii yenye mvuto mkubwa hapa nchini na duniani kote, Filamu ya Royal Tour imeoneshwa na kuangaliwa na mamia ya wadau waliokuja kushuhudia tukio hili la kihistoria kwenye sekta ya Michezo nchini.
Filamu hii iliyomshirikisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan ambayo imeifungua Tanzania duniani kwenye sekta mbalimbali imewavutia wapenzi wa soka waliokuja kutazama fainali hizo.
Waziri Mchengerwa amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendelea kutumia sekta za michezo na Sanaa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake duniani kwa kuwa zimebeba idadi kubwa ya Tanzania na kuongeza kuwa sekta hizo ndiyo nguvu shawishi ya Serikali zinazowapa watanzania wengi zaidi furaha na faraja.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Heineken Nchini ambayo ndiyo mdhamini mkuu wa tukio hilo, Bi.Fatma Mnaro amesema kuwa lengo la kuonesha mubasha fainali za UEFA hapa nchini kupitia DSTv ni kutaka kuwafanya wapenzi wa soka walione shindano hilo kwa ubora wa hali ya juu kama ambavyo watakavyoshuhudia wale ambao watahudhuria mtanange huo nchini Paris nchini Ufaransa.
Aidha, Bi. Mnaro ameongeza kuwa pamoja na kurushwa mubashara kwenye Daraja la Tanzanite pia kuna sehemu mbalimbali za majiji makubwa ambazo pia zinaonesha ambazo ni pamoja na The Cask jijini Mwanza, City Pub jijini Mbeya, Arusha na Capetown Fish Market, Samaki samaki na Triple 777 jijini Dar es Salaam.