Breaking

Thursday, 19 May 2022

WAZIRI BASHUNGWA AWATAKA MA-RC, MA-DC KUSIMAMIA HUDUMA ZA DHARURA KATIKA VITUO VYA AFYA



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini nzima kusimamia kikamilifu utoaji wa huduma ya dharura katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuondoa urasimu unaochelewesha mgojwa kupata huduma.


Bashungwa ametoa maelekezo hayo Mkoani Tabora katika warsha ya Sema na Mama wakati akijibu hoja na kero ya ucheleweshwaji wa huduma kwa wagojwa katika vituo vya kutolea huduma mkoani hapo.


“Utoaji wa huduma za dharura katika vituo vya kutolea huduma za afya itolewe kwa haraka, unaweza kumuhudumia mgojwa wakati utaratibu wa kujaza taarifa na maelezo unaendelea ili kuokoa maisha yake, hivyo nawaelekeza Wakuu wa Mikoa na wilaya kusimamia utoaji wa huduma hiyo katika maeneo yao” amesema Bashungwa


Aidha, Bashungwa amesema Serikali inatambua Machinga kuwa ni sekta rasmi ndio maana imeelekeza kuwapanga katika maeneo rafiki na kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara ambapo itakuwa rahisi kuwafikia na kuwapelekea huduma mbalimbali.


Amesema tayari Serikali imewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote kushirikiana na viongozi wa Wafanyabishara wadogo kujadili na kutafuta namna bora ya kuwapanga kulingana na mazingira ya Mkoa husika yatakayowaezesha wateja wao kuwafikia.


Vile vile, Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya sita imetoa nafasi ya upekee kwa watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali kama utoaji wa mikopo na ajira ambapo asilimi 3 ya nafasi za ajira zinazotolewa zimeelekezwa kwa watu wenye ulemavu.


Pia, amesema Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa Mikopo ya asilimia 10 za halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na sasa Wakurugezi watapimwa kwa namna wanavyotenga fedha hizo kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa kuzigawa bila upendeleo kwa kuwanufaisha wahusika.


Warsha ya  Sema na Mama iliwakutanisha viongozi wa Serikali na makundi mbalimbali ya wananchi wa mkoa wa Tabora ambao ni Machinga, Wakulima, Boda boda na watu wenye mahitaji maalum na kupata nafasi ya kusikilizwa na kujibiwa moja kwa moja na viongozi hao.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages