Breaking

Tuesday, 17 May 2022

WAZIRI BASHUNGWA ATOA MAAGIZO HOJA ZA CAG, AWATAKA MA-DED WA HALMASHAURI 7 KUJITATHMINI




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Innocent Bashungwa ametoa maagizo tisa ikiwemo wakurugenzi wa halmashauri saba zilizopata hati chafu na zenye mashaka kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kujitathimini kiutendaji.

Halmashauri hizo ni za Wilaya za Bunda, Sengerema, Kisarawe, Longido, Mlele, Musoma, na iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Pia amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango imeunda timu ya kutathimini utendaji kazi wa wakaguzi wa ndani katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa wa ambao watakuwa hawatoshi watakndolewa.

Akizungumza jijini hapa wakati akitoa taarifa ya ukaguzi wa Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2020/21 na hatua zilizochukuliwa kutekeleza maagizo ya CAG, alisema lengo ni kuhakikisha mapendekezo hayo yanatekelezwa kwa ukamilifu na dosari zinazojitokea mara kwa mara hazijitokezi tena.

Katika maagizo yake, Bashungwa ameagiza Mamlaka za Nidhamu za Waweka Hazina wa Halmashauri Saba zilizopata Hati Chafu na Hati zenye Shaka ziwachukulie hatua stahiki za kinidhamu kwa kutotekeleza ipasavyo wajibu wao kwa mujibu wa Agizo la 27(3) la Memoranda ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa – 2009.

"Waweka Hazina wana wajibu wa kutunza kumbukumbu sahihi za fedha kwa mujibu wa miongozo ili kuwezesha uandaaji wa taarifa za hesabu za mwisho."

Aidha, alimwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI awatake Wakurugenzi wa Halmashauri zote zenye hoja za ukaguzi zenye viashiria vya kutowajibika ipasavyo, pamoja na upotevu wa fedha za Halmashauri kujieleza.

Pia, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI awasiliane na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ili Taasisi hiyo iweze kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua stahiki, kwa kuwa baadhi ya hoja za ukaguzi zilizobainishwa kwenye taarifa ya CAG, zimetokana na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages