Wanafunzi 76 wa shule ya Sekondari ya Wasichana Mkuza iliyopo Kibaha wamenusurika kufa katika ajali ya moto baada ya bweni lao kuteketea wakiwa kwenye kipindi cha sala shuleni hapo huku 13 kati yao wakikimbizwa katika hospitali kwa matibabu zaidi baada ya kupatwa mshtuko.
Moto huo ambao uliozuka ghafla umeteketeza bweni la shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani usiku wa kuamkia leo Jumatatu Mei 16, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amefika katika eneo la tukio na kuwatoa hofu Wazazi wasiwe na shaka kwani Watoto wako salama na wameshapata mahali pa kuhifadhiwa, mpaka sasa tayari imeundwa Timu kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.
Kwa upande wake Marakibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani, Kamanda Jenifa Shirima amethibitisha kutokea Kwa tukio hilo na kutoa rai Kwa Wananchi kutoa taarifa Kwa wakati Ili kudhibiti moto au kupunguza athari za moto pindi unapotokea.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT Dr. Alex Malasusa ameushukuru Uongozi wa Mkoa wa Pwani pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano wao katika tukio hilo.