Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wakandarasi nchini kuendelea kutoa ushiriakiano kwa BRELA ili kuwezesha kazi zao kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Hayo yamebainishwa Ijumaa Mei 13, 2022 na Afisa Usajili wa BRELA, Gabriel Girangay wakati wa mkutano wa wakandarasi katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Girangay amesema kuwa wakandarasi ni wadau muhimu hivyo wanapaswa kutoa ushirikiano wa karibu kwani kabla ya kwenda kusajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi wanatakiwa kusajili kwanza makampuni yao BRELA.
“Wakandarasi ni watu muhimu na inapaswa kuhakikisha mnahuisha taarifa zenu kwa wakati ili muweze kutambulika kwenye mfumo na iwasaidie kushindana katika zabuni mbalimbali zinazotangazwa.” amesema Girangay
Ameongeza kuwa, wakati wa kuhuisha taarifa za wanahisa BRELA ni kiungo muhimu hivyo ni vyema kutoa ushirikiano wa kina ili kufanikisha shughuli zao za ukandarasi.
Pia amewasihi kuacha kuwatumia "vishoka" ambao wanasababisha ucheleweshaji wa michakato wa urasimishaji wa biashara.
Ameeleza kuwa, mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao ( Online Registration System-ORS) unatoa nafasi kwa kampuni kupata huduma za BRELA mahali popote.
Aidha ametoa wito kuhusu uwasilishaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa kabla ya Juni 30, 2022 ili kukidhi takwa la kisheria.