Na Samir Salum Lango la habari
Imeelezwa kuwa ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya madini umeleta Mafanikio makubwa ikiwemo ongezeko la fursa za ajira na uwekezaji katika sekta ya madini.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Mei 20, 2022 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Kwanza la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini uliofanyika jijini Mwanza na kukutanisha wadau mbalimbali wa madini.
Amesema ongezeko la ajira kwa kwa watanzania katika migodi mikubwa na ya kati ni 6,668 sawa na asilimia 95 kwa Mwaka 2018 hadi kufikia 14,308 sawa na asilimia 97 kwa Mwaka 2021 ya ajira zote.
Ameongeza kuwa katika nafasi ambazo watanzania hawajapata uzoefu kutokana na kukua kwa teknolojia serikali imeweka utaratibu wa mpango wa kushirikishwa ili watanzania wapate uwezo na kushika nafasi hizo.
"Usimamizi huu umepelekea watanzania kushikilia nafasi za uongozi katika migodi mikubwa na ya kati nchini" amesema profesa kikula
Aidha amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya watoa huduma watanzania na kampuni za kitanzania ambapo kwa mwaka 2021 jumla yake ilifikia 961 sawa na asilimia 61 ya watoa huduma wote katika kipindi hicho.
Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya Madini ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya madini Janet Lekashingo amesema kuwa kamati itaendelea kusimamia ushirikishwaji wa Watanzania na kuwapa kipaumbele ikiwemo bidhaa na huduma pamoja na kampuni za kitanzania ili kufikia lengo la ushirikishwaji na kuleta maendeleo ya kudumu.
Ameongeza kuwa Jukwaa hilo litafanyika kila mwaka ilikupima utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania na kupima changamoto na kuzitafutia ufumbuzi huku akiwaasa wananchi kutumia fursa za ajira na uwekezaji.
"wananchi wachangamkie fursa za uwekezaji katika sekta ya madini hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye madini mengi hususan ya dhahabu" amesema Lekashingo
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Tume itaendelea kutoa elimu katika maeneo mengine katika Sekta ya Madini lengo likiwa ni kuhakikisha shughuli za madini zinafanyika kwa ufanisi huku mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa ukiendelea kukua.
Awali Mwenyekiti wa Tume ya Madini alitembelea mabanda ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini na ya wadau wa madini kwenye maonesho yanayoendelea ikiwa ni sehemu ya mkutano huo.
TAZAMA HAPA: PICHA: PROF.KIKULA ATEMBELEA MAONESHO YA KWANZA YA USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI
Mkutano wa Jukwaa la Kwanza la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya madini umeanza leo Mei 20, 2022 Jijini Mwanzana unatarajiwa kufikia tamati Mei 22, 2022 ukiwa na kauli mbiu "Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya madini kwa maendeleo endelevu"