Breaking

Friday, 20 May 2022

URUSI KUSITISHA USAMBAZAJI WA GESI FINLAND


Na Said Muhibu,lango la habari 

Serikali ya Urusi imetangaza kusitisha usambazaji wa gesi asilia nchini Finland kesho Jumamosi ya Mei 21, 2022 kufuatia hatua ya Finland kuomba kujiunga na  muungano wa kijeshi wa NATO.


Kampuni ya gesi asilia inayomilikiwa na Finland, Gasum imesema kuwa imepewa taarifa ya usitishwaji wa huduma hiyo na kampuni ya shirika la nishati nchini Urusi Gazprom ijumaa ya leo hii.


 Usitishwaji wa usambazaji wa gesi ambao umeratibiwa kufanyika asubuhi ya jumamosi unakuja baada ya Finland na Sweden kutuma maombi ya kujiunga na muungano wa kijeshi wa NATO huku kukiwa na wasiwasi wa usalama uliochochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.


 Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya gesi asilia nchini Finland Milka Wiljanen, alisema katika taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo ya kwamba amesikitishwa na hatua hiyo pamoja na kuwatoa wasiwasi wananchi wa Finland ya kuwa hakutakuwa na urasimu katika sehemu nyeti kama hiyo licha ya hatua itakayochukuliwa na Urusi hapo kesho.


 "Inasikitisha sana kwamba usambazaji wa gesi asilia chini ya mkataba wetu wa usambazaji sasa utasitishwa," Alisema Wiljanen.


 "Hata hivyo, tumekuwa tukijiandaa kwa uangalifu kwa hali hii na kwa kuzingatia kwamba hakutakuwa na usumbufu katika mtandao wa usambazaji wa gesi, tutaweza kuwapa wateja wetu wote gesi katika miezi ijayo," aliongezea.


Kampuni ya gesi asilia nchini Finland, Gasum ilisema itaendelea kuwapatia wateja wa Finland gesi asilia kupitia bomba la Balticconnector linalounganisha Finland na Estonia.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages