*******
NAIBU Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhandisi, Dkt. Polite Kambamura na ujumbe wake wamesema wamejifunza usimamizi wa masoko ya madini ambayo yamesaidia kurasimisha biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo nchini Tanzania.
Mara baada ya ziara katika Mkoa wa Mwanza, Geita na Shinyanga leo Mei 25, 2022, Dkt. Kambamura na ujumbe wake wamesema wamejifunza kuhusu mwenendo wa masoko ya madini unavyofanya kazi nchini, ambao kwa kiasi kikubwa umeondoa utoroshaji wa madini kwa wachimbaji kwa kupata masoko na bei ya uhakika.
Amempongeza, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa usimamizi mzuri wa masoko ya madini ambayo yamesaidia kutokomeza utoroshaji wa madini na kuongezeka kwa mapato ya Serikali.
Amesema, lengo la ziara hiyo lilikuwa kujifunza namna wachimbaji wadogo wa madini Tanzania wanavyofanya shughuli zao ili waweze kujifunza na pia kupata uzoefu wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa Zimbabwe kuongeza ufanisi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa amemshukuru Dkt. Kambamura na ujumbe wake kwa kutembelea maeneo ya wachimbaji wadogo wa Geita na Shinyanga, masoko ya madini na kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza.
Amesema, ziara hiyo ililenga kujengeana uwezo kuhusu Sekta ya Madini inavyofanya kazi nchini ili kwa pamoja waweze kujifunza masuala mbalimbali ya usimamizi katika sekta hiyo.
Naye, Katibu wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Gregory Kibusi ameishukuru wizara kwa kutengeneza mazingira mazuri ya wafanyabiashara wa madini nchini.
Amesema, ziara ya Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe imetoa fursa kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kwenda kuchimba katika nchi yao baada ya kuhakikishiwa na Dkt. Kambamura.
Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe na ujumbe wake wamemaliza ziara ya siku tano katika mkoa wa Mwanza, Geita na Shinyanga ambayo ililenga kujifunza masuala mbalimbali katika Sekta ya Madini nchini.