Breaking

Tuesday, 17 May 2022

TUME YA MADINI YAIPIGA MSASA BancABC KATIKA UTOAJI MIKOPO KWA WACHIMBAJI MADINI NCHINI



Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amefungua semina kwa benki ya BancABC yenye lengo la kuwapa uelewa kuhusu Sekta ya Madini ili waweze kuwa sehemu ya sekta hiyo.


Mhandisi Samamba amefungua semina hiyo iliyofanyika jijini Dodoma leo Mei 17, 2022 ambayo  imeshirikisha watendaji kutoka  Tume ya Madini na Benki ya BancAB 


“Kikubwa katika semina yetu ya leo tumeongelea kuhusu masuala ya ushirikishwaji wa watanzania kwenye sekta ya madini (local content), tunafahamu mabadiliko ya sheria ya mwaka 2010 yenye lengo la kuhakikisha kwamba watanzania wanapata nafasi ya kuendeleza Sekta ya Madini” amesema Mhandisi Samamba


Aidha, amesema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa wawekezaji kwenye Sekta ya Madini wanaweza kupata mikopo nchini kupitia mabenki.


Amefafanua kuwa, kwa kuwapa uelewa mabenki kama BancABC inakuwa ni rahisi kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa wa madini huku wakiwa na matumaini kwamba fedha zao zinaweza kurudi kwa kuwa wanakuwa wameujua mnyororo mzima wa Sekta ya Madini.


Katika hatua nyingine,  ametoa wito kwa  mabenki nchini kujipanga katika kupokea wawekezaji mbalimbali wakiwemo watakaokuja kuwekeza katika Sekta ya Madini ikiwa ni matokeo ya Royal tour ambayo ameifanya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan


Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mikopo wa BancABC Salehe Ramadhani amesema kuwa wamejumuika na Tume ya Madini ili kupata mafunzo ili waweze kushiriki katika kutoa mikopo kwa wachimbaji wa madini nchini.


“Tunaishukuru Tume ya Madini kwa Mafunzo haya kwani yatakuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa mikopo tumeweza kufahamu yote yanayotakiwa kufanyika ikiwemo Sheria za Madini pamoja na Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini” amesema Ramadhani.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages