Siku mbili baada ya kuibua tuhuma za watoto 8 wenye umri kati ya miaka 6-8 kufanyiwa ukatili wa kingono na mwalimu wao katika Shule ya Msingi Global iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam zimetolewa siku 7 za uchunguzi wa kina wa tukio hilo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima amefika shuleni hapo na kutoa maelekezo hayo kwa Maafisa Ustawi Mkoa wa Dar kisha wampe ripoti ya idadi kamili ya watoto walioathiriwa na tatizo hilo.
Baada ya taarifa hizo wazazi wengine wamedai wamewahoji watoto wao waliofundishwa na mwalimu huyo mwaka jana, pia wapo waliokiri kufanyiwa vitendo hivyo na mwalimu huyo lakini walitishiwa kutosema.
Mwalimu huyo anatuhumiwa kuwabaka na kuwalawiti watoto hao ambapo baada ya kubainika Mei 25, 2022, wazazi waliwapeleka watoto Hospitali ya Mwananyamala.
Mapema kabla ya Waziri Gwajima kufika kituoni hapo baadhi ya wazazi walidai kuwa mtuhumiwa alikamatwa baada ya taarifa hizo kusambaa, lakini aliachiwa kwa dhamana na walipohoji waliambiwa mtuhumiwa ana tatizo la pumu.
Mzazi mwingine akihojiwa na ITV akasema baada ya sekeseke hilo baadhi ya walimu shuleni hapo wamekuwa na hasira na wanafunzi, ikitokea kosa kidogo adhabu inakuwa kubwa kwa mwanafunzi jambo ambalo wanaona si sawa.
Source: ITV