Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ametoa mwezi mmoja kwa TARURA Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kukamilisha ujenzi wa Daraja la Ifume.
Mhandisi Seff ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya barabara katika Mkoa wa Katavi.
“Daraja hili ni muhimu sana kwa wakazi wa hapa kwa shughuli za kiuchumi, hivyo ni lazima mhakikishe kazi hii inakamilika kwa haraka ili wananchi wa kalamsenga na Itunya waweze kusafirisha mazao yao bila kupata usumbufu unaojitokeza kwa sasa, “ alisema Mhandisi Seff.
Alisema kuwa TARURA Makao Makuu itatoa fedha ambazo alielekeza zitumike katika ukarabati wa Daraja hilo, na aliagiza tathmini ifanyike haraka na maombi ya fedha hizo yatumwe ili yafanyiwe kazi kwa haraka.
Pia ameagiza TARURA Wilaya kuhakikisha wanatoa kwa haraka magogo na uchafu wote ulioletwa na mvua na kusababisha kuziba kwa daraja hilo ili fedha zikija ukarabati ufanyike ndani ya muda wa mwezi mmoja aliotoa.
Naye diwani wa Kata ya Kapalamsenga, Mhe. Jefu Lameki ameushukuru uongozi wa TARURA kwa kusikia kilio chao kwani wamekuwa wakipata adha kubwa kutokana na kuharibika kwa daraja hilo, na kusema kuwa wanachi watashiriki kikamilifu kuondoa magogo na uchafu katika daraja hilo.
Aidha, Mhandisi Seff alifanya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Kapalamsenga -
Ifume kuelekea Bandari ya kareme Tanganyika yenye urefu wa Km 12.1 na kuridhishwa na kazi inavyoendelea, ambapo mpaka sasa ukarabati umefikia asilimia 90.
“ Barabara hii Itasaidia sana katika shughuli za usafirishaji wa mazao na pembejeo za kilimo na ni sehemu ya barabara ya kutokea bandari ya Karema hivyo ni barabara muhimu sana,” alisema Mhandisi Seff