Na John Mapelele
Serikali ya Tanzania na Qatar zimefanya mazungumzo kuratibu mashindano makubwa ya Afrika ya Soka hususan Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON ifikapo mwaka 2027.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa kwa upande wa Serikali ya Tanzania na Balozi wa Qatar nchini, Hussain Ahmad Al-Homaid leo Mei 27, 2022 Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa lengo ni kuimarisha mahusiano kwenye sekta za utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo yanalenga kusaidia Tanzania kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya michezo nchini.
Amesema kuwa tayari Serikali imeshaomba miundombinu ya soka inakayotumika kwenye mashindano ya kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika nchini Qatar ambapo Mhe, Balozi Al-Homaid amesema Serikali yake itazingatia ombi hilo kwa kuipa kipaumbele nchi ya Tanzania.
“Maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na dhamira ya Serikali kuona kuwa Tanzania inakwenda kuratibu AFCON 2027” amefafanua Mhe Mchengerwa.
Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuboresha na kujenga miundombinu ya kisasa ikiwa ni pamoja na viwanja vitatu ambayo vitasaidia Tanzania kufuzu vigezo vya kupata nafasi ya kuratibu mashindano haya.
Aidha, katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi yetu na Qatar, amesema Wizara inakwenda kuandaa tamasha kubwa la wasaanii ikiwa ni pamoja na wasanii wa uchoraji na uchongaji ambapo amefafanua kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya wasanii ambao wamekuwa wakitengeneza kazi nzuri zinazouzwa kwa thamani kubwa duniani.
Baada ya mazungumzo hayo ambayo Waziri Mchengerwa akiambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Saidi Yakubu na Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusufu Singo alipata fursa ya kukagua miundombinu ya Uwanja wa Benjamini Mkapa na Mashindano ya Afrika ya Riadha ambayo yamekuwa yakiendelea uwanjani hapo.