Na John Mapepele
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Nchi ya China zimetiliana Saini mkataba wa makubaliano ya kusaidiana katika kuboresha maeneo makuu manne ya Utamaduni, Sanaa Utalii pamoja na Elimu.
Utiaji wa Saini wa mikataba hiyo umefanyika leo Alhamisi Mei 26, 2022 na kuongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed hengerwa kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Balozi wa China nchini Wang Ke kwa upande wa Serikali ya watu wa China kwenye Ofisi ya Ubalozi wa China jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia kuhusiana na manufaa ya mikataba hiyo, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania imesaini mikataba hiyo ya ushirikiano inatarajia kuleta mapinduzi makubwa kwenye nyanja zote nne.
Amesema kwa upande wa utamaduni kutakuwa na kupeleka wadau wa utamaduni, sanaa na michezo katika nchi ya china na watu wa china kuja nchini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wa elimu Tanzania itapeleka wanafunzi ambapo China itafadhili masomo haya kwa kutoa nafasi 120 kwenda kwenye maeneo ya lugha, utamaduni, sanaa na maeneo mengine ya hinsia (humanities) kila mwaka ambapo Tanzania itatoa ufadhili wa nafasi 15 kwa ajili ya wachina kuja Tanzania kusoma hasa kwenye maeneo ya hinsia(humanities) pamoja na maeneo ya lugha.
Amesema mkataba huu unatarajiwa kutoa nafasi kwa wataalam kwenye maeneo ya sekta hizo zote. Pia imeelezwa kuwa Serikali ya China inatarajia kujenga vituo vya kisasa vyenye miundombinu yenye viwango vya kimataifa vya sanaa na utamaduni ambavyo vitatumika na wasanii wa hapa nchini katika kuzalisha kazi zao zenye ubora ambazo zitauzwa duniani.
“Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kuwa wasanii wetu wanakwenda kupata studio za kisasa kabisa kwa ajili ya kuzalisha kazi zao”amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Aidha Waziri Mchengerwa amesema Tanzania inaamini kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na utamaduni uliosheheni vitu vingi kutokana na kuwa na makabila ambayo ni zaidi ya 120.
Ameongeza kuwa kulingana na mikataba hiyo Serikali za nchi zote zinakusudia kuchangamsha utamaduni na sanaa ili ziwe kwenye kiwango halisi tofauti na sasa ambapo inaonekana kuwa kutochangamka kwa kiwango hicho.
Katika ziara hiyo Waziri Mchengerwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi na Wakurugenzi wa Sekta za Utamaduni na Sanaa kwenye Wizara hiyo, ambapo kwa Serikali ya China Mhe. Balozi Wang Ke ameambatana na watendaji waandamizi kwenye sekta hizo.