Breaking

Thursday, 26 May 2022

TANZANIA, CANADA KUWEKA MKAZO AGENDA YA KIZAZI CHENYE USAWA


Na Mwandishi Wetu

Tanzania na Canada zimejipanga kuhakikisha zinachochea maendeleo na ustawi kwa kujikita katika kutekeleza malengo ya jukwaa la kizazi chenye usawa katika eneo la pili la uwezeshaji haki za kiuchumi kwa wanawake ikiwa ni pamoja na kushughulikia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. 


Hayo yamebainika leo Mei 26, 2022 jijini Dar Es Salaam wakati wa kikao kati ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima  na Katibu wa Bunge la Canada Mhe. Robert Orifant.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kutekeleza Agenda hiyo na Rais Samia amekuwa kinara katika utekelezaji wake.


Kwa upande Katibu wa Bunge la Canada Mhe. Robert Orifant alisema, wanafurahia kuona Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kupiga hatua kwenye maendeleo yenye usawa wa kijinsia hivyo, Canada iko tayari kushirikiana na Tanzania kufanya kazi pamoja kwenye maeneo yanayolenga kwenye maendeleo ya wanawake.


Aidha Viongozi hao wamejadiliana kuhusu mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Canada hususan katika masuala ya maendeleo ya Jinsia na uwezeshaji wa Wanawake.


Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inaendelea kukutana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha inaweka mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia Sera na Mipango iliyopo.



MWISHO

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages