Breaking

Tuesday, 10 May 2022

SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI 100 KUDHIBITI UPANDAJI BEI YA MAFUTA NCHINI




SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati imetoa kauli bungeni kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta kwa lengo la kudhibiti upandaji wa bei ya nishati hiyo, miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na serikali kutoa ruzuku ya Sh.bilioni 100 katika kipindi cha mpito.

Akizungumza leo Mei 10, 2022, Bungeni Mjini Dodoma Waziri wa Nishati Januari Makamba ameliambia Bunge kuwa, katika kikao cha 16 cha Mkutano wa Saba (7) wabunge walijadili kuhusu ongezeko la bei ya mafuta nchini na kutoa maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali.

Amesema baada ya mjadala Spika ulitoa maelekezo kwamba, kwa mujibu wa Kanuni ya 56 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Serikali itoe kauli rasmi Bungeni kuhusu hatua za kupunguza athari za kupanda kwa bei za mafuta nchini.

“Napenda kuchukua hatua hii kuwajulisha kuwa Rais samia Samia Suluhu Hassan alituita na kutuketisha kitako sisi wasaidizi wake tukiongozwa na Waziri Mkuu. Mheshimiwa Rais alizungumza mengi, kwa uchungu mkubwa sana.

“Ameguswa sana na malalamiko na masononeko ya wananchi juu ya kupanda kwa gharama za mafuta na gharama za bidhaa na maisha kwa ujumla. Akasema, hata kama bei iko juu duniani, hata kama takwimu na namba zinaleta mantiki, lakini tutatungulize utu na huruma kwanza katika kulishughulikia suala hili.

“Bila shaka kwa wale waliomtizama katika televisheni akiongea na Taifa jana usiku mtakuwa mmeona huruma iliyojawa katika uso wake na imani katika sauti yake. Isingelikuwa uungwana wake wa kuheshimu mamlaka na mipaka ya Bunge, kauli hii ninayoitoa leo angeitoa yeye muda ule jana.

“Lakini akaniambia, maadam Bunge lilikuelekeza wewe uwasilishe taarifa, basi busara ya kiuongozi inataka Bunge lisikie taarifa hii kutoka kwako. Hivyo amenituma kuja kwenu leo kuwaletea habari njema.Kabla sijaufikisha ujumbe huo na kueleza hatua ambazo Serikali inachukua kwenye suala hili, ili kuongeza uelewa na kujenga muktadha.

“Ni vyema nikaeleza mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia na kutoa mnyambulisho wa gharama zinazojumuishwa katika kukokotoa bei za mafuta.Nchi yetu haina visima vya mafuta wala mitambo ya kuchakata mafuta ghafi. Kama zilivyo nchi nyingi, sisi ni wapokeaji wa bei. Kwa maana hiyo,”amesema Makamba.

Ametoa mfano kwa mafuta ya dizeli, mchango wa bei katika soko la dunia kwenye bei ya mwisho ya mlaji ulikuwa ni asilimia 64 mwezi huu. Na bei za mafuta katika soko la dunia zinatokana na uzalishaji au upatikanaji wa mafuta ghafi (crude oil), upatikanaji wa mafuta yaliyochakatwa na mahitaji ya mafuta.

Pamoja na ufafanuzi wa kina ambao Waziri Makamba ameutoa bungeni kuhusu hali ya upatikanaji mafuta katika soko la Dunia ambayo, amesema kutokana na mahitaji ya wananchi, maoni na ushauri wa Wabunge, maelekezo ya CCM na ujasiri wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais alitoa maelekezo kwamba mwaka ujao wa fedha ni mbali.

Akataka ahueni itafutwe mapema zaidi. Hivyo basi, kama hatua ya dharura Rais ametoa maelekezo kwamba, katika kipindi hiki kabla hatujafikia mwaka mpya wa fedha, Serikali ijibane na ijinyime na zitolewe Sh.bilioni mia moja kwa ajili ya kupunguza bei za mafuta hapa nchini. Ruzuku hiyo inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22.

Ameongeza kutolewa kwa ruzuku hiyo hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea. Nafuu nyingine inayotokana na mikopo aliyoeleza awali itakuja katika mwaka ujao wa fedha itaelezwa kwa kina zaidi na Waziri wa Fedha kwenye Bajeti ya Serikali mwezi ujao.

“Ruzuku hii ya Sh,bilioni bilioni 100 itatolewa kwa ajili ya kupunguza bei kuanzia Juni 1, 2022. Hii ni kutokana na kuwa, wafanyabiashara wa jumla wamekwisha lipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei hizi za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wamekwishanunua mafuta kwa bei hii inayotumika sasa.

“Hatua nyingine zisizo za kifedha zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu kufanya hivyo. Wizara imekamilisha kufanya tathmini ya kampuni zote zilizoonesha nia ya kuweza kuleta mafuta kwa bei nafuu kwa lengo la kujiridhisha na uwezo wao wa kuleta mafuta hayo ili kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini,”amesema.


Amesema mipango hiyo ikileta matokeo yanayotarajiwa, bei za mafuta zitapungua zaidi kuanzia mwezi Agosti 2022.Pia kuanzisha Mfuko wa Kuhimili Ukali wa Bei za mafuta (Fuel Price Stabilization Fund). Serikali imeandaa utaratibu wa kuanzisha mfuko maalumu utakaotumika kupunguza makali ya bei ya mafuta kipindi ambacho bei hizo zinaongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Mpango wa kuanzisha mfuko huu uko katika hatua za mwisho za maandalizi na utakapokamilika, utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri.Kuanzisha Hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati (National Strategic Petroleum Reserve). Serikali inakamilisha marekebisho ya Kanuni za kuanzisha na kuendesha hifadhi mafuta ya kimkakati ili nchi yetu ijihakikishie usalama wa upatikanaji wa mafuta na unafuu wa bei katika vipindi kama hivi.

“Kuwa na kituo kikubwa cha mafuta (Petroleum Hub). Serikali inakamilisha makubaliano ya kujenga maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta kwa ajili ya kuuzwa ndani na nje ya nchi kulingana na uhitaji. Uwepo wa kituo hiki utawezesha nchi kupata mafuta yenye bei nafuu pale bei zinapopanda kupita kiasi.Mpango huu na utekelezaji wake unaweza kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu,”amesema Waziri Makamba

Ameogeza hatua nyingine ni kuanzisha upokeaji wa mafuta katika ghala moja (Single Receiving Terminal – SRT) kupitia maghala ya TIPER ili kupunguza au kuondoa gharama za meli kusubiri au kuchukua muda mrefu katika upakuaji wa mafuta katika maghala mengi.

Amesema gharama hizo nazo zina mchango katika bei ya mafuta (demurrage charges). Hatua hii itaondoa changamoto za udanganyifu na kuongeza ufanisi katika biashara ya mafuta hapa nchini. Hatua hii inaendana na kuyafanya maghala haya kuwa Customs Bonded Warehouse ili kushamirisha biashara ya mafuta yanayokuja nchini na kwenda kwenye nchi nyingine.

Pia kuiongezea uwezo TPDC kuagiza mafuta nje ya nchi, ambapo kwa mara ya mwisho ilifanya shughuli hiyo miaka 20 iliyopita.Hatua nyingune ni kuimarisha utendaji na weledi wa taasisi za Serikali zinazoshughulika na biashara ya mafuta nchini, ikiwemo EWURA na PBPA (Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja).

“Hatua hizi zitafafanuliwa kwa kirefu na fursa ya Wabunge kutoa maoni na ushauri wao wakati wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati wiki tatu zijazo.Bunge lako litakuwa limebaini changamoto za foleni na vurugu katika vituo vya mafuta zilizopo katika nchi nyingine zinazotokana na uhaba wa mafuta.

“Pamoja na changamoto ya bei, ambalo sio suala letu peke yetu, usimamizi wa sekta ya mafuta hapa nchini, hasa katika kipindi hiki kigumu, umekuwa wa utulivu na wa umakini. Hii sio kwasababu ya ajali bali ni kwa jitihada za makusudi za Serikali kwa ushirikiano na sekta binafsi.

“Bei za mafuta kupanda ni janga lakini hatari kubwa zaidi hata kwa usalama wa nchi ni kukosekana kwa mafuta. Hili halijatokea hapa kwetu na hatutaruhusu litokee. Leo tunapozungumza tunayo petroli ya kutosheleza kwa mahitaji ya siku 34, dizeli ipo ya kutosheleza kwa mahitaji ya siku 27, mafuta ya taa kwa siku 81 na mafuta ya ndege kwa siku 26.

“ Haya ni mafanikio kwani sote tunafahamu kwamba zipo nchi zimelazimika kutaifisha mafuta ya nchi nyingine yanayopitia kwao kutokana na uhaba. Serikali inawapongeza wadau wa mafuta nchini, hasa kupitia vyama vyao vya TAOMAC na TAPSOA, kwa uelewa wao, ushirikiano wao na uvumilivu wao katika kipindi hiki.”

Aidha amesema Serikali pia inaishukuru Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa ushauri mzuri ambao imekuwa inautoa kwa Wizara katika usimamizi wa sekta. Pia ametoa kwa Bunge kuchukua nafasi yake kwenye kuisimamia na kuishauri Serikali kwenye suala hilo.

“Kipee nimshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake na ujasiri wake wa kuchukua hatua ambayo tumeilezea hapa leo. Ni dhahiri kabisa kwamba, yeye binafsi na Serikali yake na Chama anachokiongoza, wanawajali wananchi na wanatoa majawabu kwa mahitaji yao,”amesema Makamba




Source:
Michuzi Blog
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages