Breaking

Thursday, 26 May 2022

SERIKALI YATANGAZA KANUNI MPYA YA MAFAO YA PENSHENI




Serikali imetangaza rasmi Kanuni mpya ya Mafao ya mkupuo ambapo sasa ni 33% kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii.


Kanuni hiyo imetangazwa leo Alhamisi Mei 26, 2022 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu Jijini Dodoma.


Prof. Katundu amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan baada ya kuridhia maombi ya wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii ikijumuisha wawakilishi wa Wafanyakazi (TUCTA), Waajiri (ATE) na serikali kwa kupandisha asilimia ya kikokotoo kutoka asilimia 25 iliyolalamikiwa mwaka 2018 mpaka asilimia 33.


Ameelezea kuwa Kanuni hiyo mpya ambayo imetangazwa ina manufaa mengi ikiwemo Mifuko ya pensheni ya PSSSF na NSSF kuimarika na kuwa endelevu, kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kutoka asilimia 25 iliyokataliwa mwaka 2018 hadi asilimia 33, kuongeza pensheni ya mwezi kutoka asilimia 50 ya sasa hadi asilimia 67 kwa waliokuwa wanachama wa PSPF na LAPF ambao ni asilimia 19 ya wanachama wote wa Mifuko ya pensheni.


Ameongeza kuwa mifuko itaweza kuongeza pensheni ya kila mwezi kwa kuzingatia tathimini zitakazofanyika kila baada ya miaka mitatu.


Aidha Wanachama wote wanaochangia kwenye Mifuko ya pensheni watatumia kanuni moja ya mafao na hivyo kuweka uwiano na usawa wa mafao baina ya Wastaafu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages