Breaking

Sunday, 29 May 2022

SERENGETI GIRLS YATAKIWA KUIPA HESHIMA NCHI KWA KUSHINDA MCHEZO WA MARUDIANO NA CAMEROON


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema watanzania   wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan wanaitaka timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) kuleta ushindi wa heshima katika mechi ya marudiano dhidi ya timu ya Cameroon ili kufuzu mashindano ya soka ya dunia.


Serengeti Girls ilishinda mabao manne kwa nunge  kwenye mechi ya awali Mei 22, 2022 nchini Cameroon. 


Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo alipoitembelea timu hiyo akiambata na Naibu Waziri wake, Pauline Gekul, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi na Mkurugenzi wa Michezo nchini pamoja na Viongozi  Wakuu wa Shirikisho la soka Tanzania na Zanzibar kwenye uwanja wa Amani uliopo Zanzibar.

Amesema  kuwa watanzania wanaimani kubwa na timu hiyo ili kuandika historia  ya  kuwa timu ya kwanza Tanzania kufungua  milango ya Tanzania kuingia mashindano ya dunia mwaka huu.


“Na msikubali kufungwa hata goli moja kwenye mechi hii na huo ndiyo ushindi wa heshima, na heshima hii mtaipeleka kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar. Mhe, Dkt. Hussein Mwinyi na watanzania wote kwa ujumla” amesisitiza  Mhe. Waziri Mchengerwa


Amesema ndoto ya Rais Samia ni kuona kuwa timu hiyo inapiga hatua kwenye mchezo huo ili kulipeleka taifa la Tanzania kwenye mashindano ya dunia na amewaomba kuweka uzalendo na utaifa mbele.

Amesema vipaji hiyo walivyonavyo kama wataweza kuyabeba na matumaini ya watanzania walio wengi wenye hamu ya kujua kitachoitokea katika mchezo ujao basi mtaji wao ni vipaji vyao wao kwa maana ya kuwa  vipaji vyao ndiyo mtaji wao wa kufungua na kuboresha maisha yao. 


Aidha, ameeleza kuwa watanzania wengi wamekuwa na hofu kuwa Tanzania haiwezi kupiga hatua kwenye soka pengine kwa sababu hakuna miundombinu ambapo amesema  hiyo siyo kweli kwa kuwa  timu hiyo imefika kwenye hatua hiyo ya juu kabisa kwa  kutumia miundombinu hiyohiyo.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Pauline Gekul amewapongeza wachezaji   hao na kuwataka kuendelea kuwasikiliza walimu wao ili kufika  mbali zaidi kwenye mashindano ya kimataifa.

Naye Nahodha wa timu hiyo, Nohela Luhala amemthibitishia Mhe. Waziri na ujumbe wake  kuwa watapambana kufa na kupona ili kuhakikisha kuwa wanaingia kwenye mashindano hayo ambayo yatafanyika nchini India  mwaka huu. 


“Ninaomba kukuhakishia Mhe. Waziri kuwa kama Mhe. Mama yetu kipenzi na Rais wetu Samia Suluhu Hassan alivyokuwa Rais Mwanamke wa kwanza kuiongoza Tanzania na sisi itakuwa timu ya kwanza nchini kuiingiza Tanzania kwenye mashindano ya dunia ya soka” amesisitia Luhala.   

 Awali Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi amesisitiza kuendelea kufanya jitihada  zaidi  kweny mchezo unaofuata huku wakimtegemea  mwenyezi mungu huku Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusufu Omary Singo amesema  timu hiyo imekuwa na nidhamu kubwa ukilinganisha na timu nyingine za soka na kwamba imechaguliwa kuiwakilisha Tanzania kwenye michezo ya Olympik  nchini Ufaransa. 


Rais wa Shirikisho la soka Zanzibar Abdiratifu Ali Yasin ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa mahusiano mazuri ya kuunganisha mashirikisho, vyama vya michezo na Serikali kwenye michezo.


Katika ziara hiyo Mhe. Mchengerwa na ujumbe wake walikula chakula cha pamoja na timu hiyo

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages